‘Wanataaluma wazingatie uadilifu matumizi akili unde’

MBEYA; Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Munde, amesema matumizi ya Akili Unde (AI) katika taaluma mbalimbali, ikiwemo uhasibu, yanapaswa kwenda sambamba na uadilifu na weledi wa kitaalamu, akionya kuwa teknolojia hiyo haiwezi kuchukua nafasi ya uwezo wa binadamu kufanya maamuzi sahihi.

Amesema licha ya AI kuwa na uwezo wa kurahisisha uchambuzi wa taarifa, kuongeza ubunifu na kubaini viashiria vya udanganyifu, bado kuna mambo yanayohitaji uamuzi, uzoefu na uadilifu wa kitaalamu wa binadamu.

Munde ametoa wito huo alipokuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 24 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Mbeya, ambapo jumla ya wahitimu 1,736 wakiwemo wa cheti cha awali,stashashada na shahada ya kwanza wamehitimu katika mahafali hayo.

“Tumieni teknolojia kwa ubunifu na uadilifu, lakini msiruhusu ifikiri kwa niaba yenu,kuna mambo maalumu ambayo AI haiwezi kuyabaini wala kuyabuni,” amesema Munde, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya taaluma katika matumizi ya teknolojia.

Aidha amewataka wahitimu walionufaika na mikopo ya elimu ya juu kuanza kurejesha mikopo hiyo mara wanapoanza kupata ajira au kipato kupitia shughuli za kujiajiri, ili kuwawezesha vijana wengine kupata fursa ya mikopo hiyo na kuendelea na masomo ya elimu ya juu.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Pallangyo, jumla ya wahitimu 1,736 wamehitimu katika Kampasi ya Mbeya, wakiwemo wanawake 881 na wanaume 855 ,ikiwa ni ongezeko la asilimia 17.3 ikilinganishwa na wahitimu 1,480 wa mwaka wa masomo 2024/2025.

Profesa Pallangyo ameongeza kuwa jumla ya wanafunzi 2,158 wa Kampasi ya Mbeya wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.7, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22.3 ikilinganishwa na wanafunzi 1,765 walionufaika katika mwaka uliotangulia wa masomo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri ya TIA, Profesa Jehovaness Aikael, amewataka wahitimu kujenga uwezo wa kufanya kazi kwa ushirikiano, kuheshimu mawazo tofauti, kusimamia fedha na kutumia fursa zilizopo kujitegemea kiuchumi.

Mhitimu wa Shahada ya Masoko kwa Jamii, Saidi Mtunga amesema licha ya akili unde(AI) kuwasaidia wataalamu kupata mawazo mapya na kupanua wigo wa maarifa, lakini matumizi yake yanahitaji umakini ili kupata matokeo chanya.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button