Watakiwa kuimarisha usimamizi watoto wanaohitimu shule

KILIMANJARO; Wazazi wametakiwa kuimarisha usimamizi wa malezi ya watoto hata baada ya kuhitimu masomo, kutokana na kuongezeka kwa changamoto zinazoweza kuhatarisha mustakabali wa vijana, zikiwamo matumizi yasiyodhibitiwa ya mitandao ya kijamii, ushawishi wa makundi mabaya ya marafiki, dawa za kulevya na mahusiano ya kimapenzi ya mapema.
Akizungumza katika mahafali ya tano ya wanafunzi wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari New Dawn, iliyopo wilayani Same, Askofu Mkuu wa Kanisa la Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT), Stevie Mulenga, amesema jukumu la mzazi halipaswi kuishia mtoto anapohitimu shule au kuanza kujitegemea, bali linapaswa kuendelea kwa kumshauri, kumfuatilia na kumsaidia kufanya maamuzi sahihi yanayolinda maisha na mustakabali wake.
Amesema kumaliza shule ni mwanzo wa safari nyingine ya maisha yenye changamoto zinazohitaji maamuzi sahihi, akiwataka vijana kutambua kuwa wanapovua sare za shule hawapaswi kuvua nidhamu, kwa kuwa ndiyo itakayowalinda wanapoingia katika jamii.
“Unapovua sare za shule na kuvua nidhamu, umeanza maisha. Sare ni kitambaa unachoweza kukivua, lakini nidhamu ni tabia uliyoivaa kwa miaka minne. Ukiivua, unabaki mtupu na maisha ya nje duniani huko hayana huruma kwa mtu asiye na maadili,” amesema.
Ameeleza kuwa shuleni wanafunzi walikuwa na walinzi wanne, ambao ni sare, kengele, walimu na uzio wa shule, lakini baada ya kuhitimu wanapaswa kujilinda wenyewe kwa kutumia nidhamu waliyojengewa.
Amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kuchagua marafiki kwa umakini, kuepuka mahusiano ya mapema, kutumia simu na mitandao ya kijamii kwa manufaa, kujifunza kujitegemea, kufanya kazi na kuweka akiba.
Aidha, amewataka kutokubali hofu, tamaa, kujilinganisha na wengine wala kukata tamaa wanapokutana na changamoto, akisisitiza kuwa mafanikio yanahitaji uvumilivu na bidii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa shule hiyo, Dk Stephen Mshomi, amewataka wazazi kuendelea kusimamia malezi ya watoto hata wanapohitimu Kidato cha Nne, Kidato cha Sita au kujiunga na vyuo.
Amesema baadhi ya changamoto za kitabia zinazowakabili vijana zinatokana na wazazi kutotekeleza ipasavyo nafasi yao katika malezi.
Naye Mwenyekiti wa Wazazi, Zakayo Mosha, amewataka wazazi kuwapokea na kuwalea vizuri watoto wanaporejea nyumbani baada ya masomo, huku akiiomba Serikali na wadau kusaidia shule hiyo kupanua wigo wa elimu kwa kuanzisha kidato cha tano na kita, pamoja na taasisi ya sayansi na teknolojia.

Amesema shule hiyo imekuwa msaada kwa watoto yatima na familia zisizojiweza kwa kuwapatia elimu ya sekondari bila malipo.
Akitoa taarifa, Mkuu wa shule, Emmanuel Kitadu, amesema wanafunzi 38 wamehitimu kidato cha nne, huku akieleza kuwa shule hiyo inatoa elimu bure kwa watoto yatima, watoto wa mazingira magumu na wanaotoka familia zisizojiweza.
Shule hiyo pia inawapatia chakula, malazi na mahitaji ya shule, pamoja na kuwajengea misingi ya kiroho, kitaaluma, maadili na nidhamu.
Katika hatua nyingine, Dk Mshomi ameiomba mamlaka za maji kutathmini gharama za huduma hiyo, ambazo amesema zimeongezeka na kuwa mzigo kwa wananchi.

Pia, ameeleza kuwa uvamizi wa tembo katika eneo la shule na makazi ya wananchi umekuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira, miti na mali.
Akijibu changamoto hizo, Diwani wa Kata ya Njoro, Omary Abdalla, amesema Serikali inaendelea na operesheni za kuwafukuza tembo, akieleza kuwa hatua hiyo itakuwa endelevu kutokana na wanyama hao kurejea baada ya kufukuzwa.



