BOOST yavuka lengo, madarasa 16,000 yajengwa, 51 chakavu yakarabatiwa

MWANZA: SERIKALI imetekeleza Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) kwa asilimia 140, mafanikio yaliyovuka lengo la awali baada ya kutumia takribani Sh trilioni 1.15 katika kipindi cha miaka minne ya utekelezaji.

Mradi huo unaotarajiwa kufikia tamati Desemba 30 mwaka huu, umewezesha ujenzi wa madarasa zaidi ya 16,000 dhidi ya lengo la awali la madarasa 12,000, sambamba na ukarabati wa shule chakavu, ujenzi wa shule mpya na uwekezaji katika teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

Mafanikio hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Festo Dugange, alipokagua miundombinu iliyojengwa kupitia mradi huo katika Shule za Msingi Samia, wilayani Nyamagana na Kigongo, wilayani Misungwi, mkoani Mwanza.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kuelekeza uwekezaji mkubwa katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, ikiwemo matumizi ya teknolojia za kisasa.

Dk. Dugange alisema kati ya fedha zilizotolewa kupitia mradi huo, Sh bilioni 237.9 zimetumika kukarabati shule za msingi chakavu 1,059, hatua iliyolenga kuboresha mazingira ya wanafunzi na walimu.
Aidha, alisema Sh bilioni 53.9 zilitumika kukarabati shule za msingi 369 na kujenga upya shule 51 zilizokuwa katika hali chakavu.

Alisema uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia, kuongeza ufanisi wa ufundishaji na kuboresha ubora wa elimu nchini.

Mradi wa BOOST ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya elimu, ukiwa na lengo la kupanua upatikanaji wa elimu bora kwa kuboresha miundombinu ya shule za awali na msingi nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button