Ubunifu wafungua soko jipya la bidhaa za mkonge

ARUSH: Ubunifu wa vijana katika kutumia zao la mkonge kutengeneza bidhaa mbalimbali unaibua fursa mpya za kujiajiri na kuongeza thamani ya zao hilo nchini.
Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ibrahim Metu, amesema ushirikiano na Bodi ya Mkonge umemwezesha kutumia malighafi hiyo kubuni na kutengeneza bidhaa zinazoweza kutumika majumbani na hotelini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya Jukwaa la Horti Logistica Africa yanayofanyika kwenye viwanja vya TGT jijini Arusha, Metu amesema miongoni mwa bidhaa anazotengeneza ni saa za ukutani, vikapu vya kuhifadhia mazao ya chakula kama karoti, hoho na nyanya, pamoja na mazulia.
Amesema shughuli hiyo inampa nafasi ya kutumia ubunifu wake kuzalisha bidhaa zenye matumizi ya kila siku, huku ikimfungulia njia ya kujiajiri na kujipatia kipato.
“Nashukuru Bodi ya Mkonge kwa kutupa fursa sisi vijana wabunifu kutengeneza bidhaa mbalimbali kupitia zao hili. Hii ni fursa kubwa ya kujiajiri na kuongeza thamani ya mkonge,” amesema Metu.

Kwa upande wake, Ofisa Masoko wa Bodi ya Mkonge, Besti Rukanda, amesema bodi hiyo inaendelea kushirikiana na wabunifu ili kupanua matumizi ya mkonge na kuongeza thamani ya zao hilo kupitia bidhaa zinazoweza kuuzwa ndani na nje ya nchi.
Amesema ubunifu katika matumizi ya mkonge, ikiwemo utengenezaji wa bidhaa na vifungashio, unaweza kufungua fursa za kiuchumi kwa wakulima na wabunifu, pamoja na kuongeza wigo wa masoko ya zao hilo.
Ushirikiano huo unaonesha namna mazao ya kilimo yanavyoweza kuwa chanzo cha shughuli za uzalishaji na ajira zaidi ya matumizi yake ya awali, kupitia ubunifu na uongezaji thamani.



