Vifo vya wahamiaji ajali ya boti Senegal vyafikia 39

SENEGAL: Idadi ya watu waliofariki dunia katika ajali ya boti iliyokuwa imebeba wahamiaji kuelekea Visiwa vya Canary, nchini Hispania, imefikia 39 baada ya miili mingine kupatikana Jumatatu, wakati shughuli za uokoaji zikiendelea katika pwani ya Senegal.

Boti hiyo ndogo ya mbao ilipinduka katika Bahari ya Atlantiki, eneo la pwani ya Senegal kati ya mji mkuu Dakar na mji wa Saint-Louis, ikiwa safarini kuelekea Visiwa vya Canary kupitia Hispania.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Senegal (APS), ni abiria mmoja pekee aliyenusurika na kuokolewa hai, huku wengine kadhaa wakihofiwa kuwa bado hawajapatikana.

Tukio hilo limeibua tena wasiwasi kuhusu hatari zinazowakabili wahamiaji wanaotumia njia ya Bahari ya Atlantiki kutafuta maisha bora barani Ulaya.

Siku ya Ijumaa, mamlaka za Senegal zilikamata boti nyingine iliyokuwa na wahamiaji 142 kutoka nchi tano za Afrika Magharibi, hatua inayoonesha kuendelea kwa safari hizo licha ya hatari zake.

Wakati huohuo, mamlaka katika kisiwa cha El Hierro, kilichopo katika Visiwa vya Canary, zilitangaza hali ya dharura Jumamosi baada ya kupokea zaidi ya wahamiaji 3,300 waliowasili kwa kutumia takribani boti 30 tangu mwanzoni mwa Novemba.

Kuimarishwa kwa doria za baharini na Senegal, Mauritania na Morocco kumeripotiwa kusababisha baadhi ya wahamiaji kuanzia safari zao maeneo ya kusini zaidi, yakiwemo Gambia, Guinea-Bissau na Guinea, hali inayoongeza umbali na hatari za safari kuelekea Ulaya.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button