Posta yapanua uwezo kukidhi mahitaji ya wateja

DAR ES SALAAM: SHIRIKA la Posta Tanzania limeelekeza nguvu katika kuboresha uzoefu wa wateja kwa kuimarisha uwezo wa watumishi wake, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa huduma na ushindani katika soko la huduma za posta na usafirishaji.
Katika kuimarisha mkakati huo, Shirika limetoa mafunzo ya huduma kwa wateja na mawasiliano kwa mameneja wa posta kutoka mikoa mbalimbali nchini, yakilenga kuboresha usimamizi wa huduma na kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano, Huduma kwa Wateja na Mawasiliano wa Shirika hilo, Jamila Mbarouk, amesema ubora wa huduma ni muhimu katika kujenga uaminifu wa wateja na kuhakikisha Shirika linaendelea kukidhi mahitaji yao.

Amesisitiza kuwa mameneja wanapaswa kuhakikisha wateja wanahudumiwa kwa weledi, heshima na ufanisi, akieleza kuwa mahusiano mazuri na wateja ni sehemu muhimu ya ukuaji endelevu wa taasisi hiyo.
Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo hayo, Wilson Vicent Nkutigwa, amesema uwajibikaji, weledi na ubora wa huduma ni misingi inayopaswa kuzingatiwa ili kuvutia na kudumisha wateja katika mazingira ya ushindani wa kibiashara.
Ameeleza kuwa kuridhika kwa wateja, kuwasilisha mizigo kwa wakati na kutatua changamoto zinazojitokeza kwa haraka ni miongoni mwa viashiria vinavyopaswa kuongoza utendaji wa kila siku wa watumishi wa Shirika hilo.
Mafunzo hayo yanaangazia nafasi ya rasilimali watu katika kuboresha huduma za posta, wakati ushindani katika sekta ya usafirishaji na utoaji huduma ukiendelea kuhitaji taasisi kuongeza ufanisi na kuimarisha mahusiano na wateja.



