‘Wakandarasi wazembe hawana nafasi Ngara’

KAGERA: MKUU wa Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, Kanali Matias Kahabi, amesema hataacha kuwachukulia hatua za kisheria wakandarasi wanaoshindwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wakati, akieleza kuwa ucheleweshaji huo unawanyima wananchi huduma zinazotarajiwa.

Akizungumza na madiwani, watendaji na wakuu wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Kahabi amesema baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakichelewesha utekelezaji wa miradi ya maji, barabara na huduma nyingine za kijamii bila sababu za msingi.

Amesema hali hiyo haiwezi kuvumiliwa kwa kuwa Serikali imeweka rasilimali kwa ajili ya miradi hiyo, lakini wananchi wanaendelea kusubiri huduma kutokana na kutokamilika kwa kazi kwa wakati.

“Kwa muda ambao nimemaliza miaka sita ya kuwatumikia wakazi wa Ngara, nimejifunza mambo mengi, ikiwemo wakandarasi kuchelewesha miradi bila sababu za msingi. Nataka niwahidi kuwa mimi sinunuliki wala sihongeki. Nitawasweka ndani na tutaenda kwa kasi ileile, hakuna kulala, wananchi wanataka huduma,” amesema Kahabi.

Katika hatua nyingine, Kahabi amepongeza utaratibu unaotumiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Solomon Kimilike, wa kutumia siku nne hadi tano kwa wiki kupeleka wakuu wa idara na wasaidizi wao katika maeneo mbalimbali ya wilaya kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

Amesema Ngara itaendelea kushirikiana na watendaji na wadau mbalimbali kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, hususan katika sekta za mifugo na kilimo, ili kuvutia wawekezaji na kuongeza shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Wilbard John Bambarara, amesema baraza la madiwani kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji limeweka vipaumbele vitatu, ambavyo ni kuongeza mapato ya Halmashauri, kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza hoja za ukaguzi katika shughuli za halmashauri.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button