Takukuru, World Vision kudhibiti rushwa miradi ya maendeleo

ARUSHA: TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeingia makubaliano ya ushirikiano na Shirika la World Vision Tanzania kwa lengo la kuimarisha udhibiti wa rushwa, kulinda rasilimali na kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispian Chalamila, amesema makubaliano hayo yataweka mfumo rasmi wa ushirikiano katika kutoa elimu, kubaini mianya ya rushwa na kuchukua hatua dhidi ya wanaokiuka sheria na taratibu.
Amesema ushirikiano huo utajikita katika maeneo mawili makuu ambayo ni kutoa elimu na kujenga uwezo kuhusu vitendo vya rushwa na madhara yake, pamoja na kuimarisha mifumo ya kuzuia rushwa katika shughuli za World Vision Tanzania.

Katika eneo la elimu, amesema taasisi hizo zitashirikiana kuandaa mafunzo, semina, warsha na vipindi vya uhamasishaji kwa watumishi, viongozi, washirika, wazabuni na wanufaika wa miradi ya shirika hilo.
Ameongeza kuwa elimu hiyo itahusisha utambuzi wa makosa ya rushwa, madhara yake na athari za kisheria, huku ikilenga kukuza maadili, uadilifu na uwajibikaji pamoja na kuelimisha jamii kuhusu njia za kutoa taarifa za vitendo vya rushwa.

Katika kuimarisha mifumo, Chalamila amesema TAKUKURU itashirikiana na World Vision kufanya tathmini ya viashiria vya hatari ya rushwa katika usimamizi wa fedha, manunuzi, shughuli za kiutendaji na mikataba ya ushirikiano.
Aidha, TAKUKURU itatoa ushauri wa kitaalamu kuhusu mifumo ya udhibiti wa ndani, mgawanyo wa majukumu, udhibiti wa migongano ya maslahi na uzingatiaji wa maadili katika michakato ya manunuzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa World Vision Tanzania, James Nditi, amesema shirika hilo limekuwa likihudumia watoto na jamii nchini kwa zaidi ya miaka 40 na limejizatiti kuhakikisha kila rasilimali inayokabidhiwa kwake inatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.

Amesema mazungumzo ya awali kati ya taasisi hizo yalibaini kuwa zina dira na misingi inayofanana katika kukuza uwazi, uadilifu na uwajibikaji, hali iliyowezesha kuandaa mfumo rasmi wa ushirikiano uliozaa makubaliano hayo.
Nditi ameeleza kuwa ubadhirifu au matumizi ya rasilimali nje ya malengo yaliyokusudiwa yanaweza kuwaathiri watoto walio katika mazingira magumu, kudhoofisha imani ya wananchi na kurudisha nyuma maendeleo ya jamii.

Amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kulinda rasilimali zinazokusudiwa kuboresha maisha ya watoto, familia na jamii za Kitanzania.



