‘Kila mmoja aanze usafi nyumbani kwake’

DAR ES SALAAM: MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wakazi wa mkoa huo kuanza kudumisha usafi kuanzia majumbani mwao, kuwa mabalozi wa usafi na kukemea tabia ya utupaji holela wa taka ili kuboresha mazingira na kulinda afya za wananchi.
Chalamila ameyasema hayo leo, Novemba 14, 2026, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Usafi iliyoambatana na ugawaji wa vifaa vya usafi, uliofanyika katika Viwanja vya Posta, Kijitonyama, Dar es Salaam.
Amesema Dar es Salaam inakabiliwa na changamoto za uchafuzi wa mazingira unaotokana na utupaji holela wa taka, kuziba kwa mitaro, uchafu katika masoko na fukwe, hali inayoharibu taswira ya mkoa na kuhatarisha afya za wananchi.

Amesema mkoa huo huzalisha takribani tani 4,600 za taka, hivyo ni muhimu kwa kila mkazi kushiriki kikamilifu katika kuzifanya mazingira kuwa safi.
“Dar inazalisha taka tani 4,600, sasa tunasema inatosha. Niwaombe watu wote waendelee kutambua kuwa mkoa huu hakuna mwingine wa kuusafisha, ni jukumu letu sote,” amesema.
Amesema kampeni hiyo inalenga kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa safi wakati wote, hususan kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 na mikutano mbalimbali ya kimataifa inayotarajiwa kufanyika nchini.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa usafi haupaswi kuwa zoezi la maandalizi ya matukio makubwa pekee, bali uwe sehemu ya maisha ya kila siku ya wakazi wa mkoa huo.
Amesema kampeni hiyo haina mwisho kwa kuwa inalenga kujenga na kuendeleza utamaduni wa usafi kwa jamii, ndiyo maana kauli mbiu yake inasisitiza kuwa usafi ni jukumu la kila mmoja.
Aidha, amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akielekeza juhudi za kuboresha usafi Dar es Salaam kutokana na kuwepo kwa maeneo yenye uchafu, hivyo mkoa umeweka mikakati na malengo ya kukabiliana na changamoto hiyo.
“Pia, tumeshapata mwekezaji wa dampo la Pugu aliyetoka nchini Ghana atakayechakata taka,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam, Razalous Mwakiposa, amesema mitaa yote 564 imejipanga kushiriki katika kampeni hiyo ili kuhakikisha mkoa unakuwa safi.
Naye Mwenyekiti wa Makandarasi wa Usafi Dar es Salaam, Mathew Andrew, amesema ushirikiano kati ya wadau ni muhimu katika kufanikisha azma ya kuifanya Dar es Salaam kuwa safi.
Hata hivyo, ameiomba Serikali kuweka mazingira rafiki kwa wakandarasi wazawa, akitaka magari yanayotumika kukusanya na kusafirisha taka yatambuliwe katika mfumo wa usafirishaji ili yaweze kutekeleza majukumu yake bila vikwazo.
“Tunaomba magari ya taka yatambuliwe katika mpango wa usafirishaji wa taka, yatambulike kama ni miongoni mwa magari muhimu hata yakiwa barabarani,” amesema.
Katika kampeni hiyo, pia kutakuwa na kundi la mabaunsa watakaosaidia kusimamia zoezi la usafi na kudhibiti wachafuzi wa mazingira. Aidha, pikipiki zimetolewa kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa kampeni katika mitaa mbalimbali ya Dar es Salaam na kutoa taarifa za maendeleo yake.



