Watanzania wahamasishwa matumizi bidhaa za ndani

DAR ES SALAAM: Watanzania wametakiwa kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa nchini kwa kuzitumia na kuzipa nafasi katika soko, hatua inayotajwa kuwa muhimu katika kukuza viwanda vya ndani, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi.

Wito huo umetolewa na kampuni ya Tarmol Industries wakati wa uzinduzi wa bidhaa mpya za usafi na urembo, ikiwamo sabuni ya maji ya kuogea, shampoo, dawa ya kusafishia magari na bidhaa za kusafisha vyoo na vigae.

Meneja Masoko na Mauzo wa kampuni hiyo, Suzan Mkamba, amesema bidhaa hizo zimetengenezwa kwa kuzingatia mahitaji ya watumiaji wa Tanzania, ikiwamo mazingira ya hali ya hewa na aina mbalimbali za ngozi.

Akizungumza katika uzinduzi wa bidhaa hizo jijini Dar es Salaam leo Jumapili, Novemba 15, 2026 amesema kampuni inalenga kuwapatia Watanzania bidhaa zenye ubora na bei zinazoweza kumudu makundi mbalimbali ya watumiaji, huku ikipanua wigo wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Mkamba amesema bidhaa hizo zinapatikana katika vifungashio mbalimbali, kuanzia pakiti ndogo za Sh300, huku baadhi zikiwa katika chupa za mililita 750 na madumu ya lita tano.

Uzinduzi huo pia umeibua fursa za kiuchumi kwa vijana wanaotaka kujishughulisha na biashara, ambapo kampuni imewahamasisha mawakala na waundaji maudhui kununua bidhaa hizo kwa bei ya jumla na kuziuza kupitia majukwaa ya kidijitali kama Instagram na TikTok.

Wito huo unakuja wakati ambapo soko la bidhaa za usafi na urembo linatoa fursa kwa wazalishaji wa ndani kuongeza ushindani kwa kuwekeza katika ubora, ubunifu, vifungashio na upatikanaji wa bidhaa kwa bei zinazomudu watumiaji.

Hata hivyo, mafanikio ya bidhaa za ndani yanategemea pia uwezo wa wazalishaji kudumisha viwango vya ubora, kuhakikisha usalama wa watumiaji na kujenga imani ya soko kupitia taarifa sahihi kuhusu viambata na matumizi ya bidhaa zao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button