Karimjee Foundation, Chuo Kikuu Glasgow wafurahia miaka 10 ya ushirkiano

DAR ES SALAAM; Karimjee Foundation na Chuo Kikuu cha Glasgow wameadhimisha miaka kumi ya Mpango wa Ufadhili wa Masomo ya Uhifadhi wa Karimjee, katika hafla iliyofanyika mwishoni mwa wiki ofisi za taasisi hiyo zilizopo Barabara ya Sokoine, Dar es Salaam.
Hafla hiyo iliwakutanisha wahitimu wa zamani na wa sasa, wawakilishi wa chuo, wadau wa uhifadhi na wanachama wa taasisi hiyo, kusherehekea ushirikiano ambao umewajenga wanasayansi wa Kitanzania wa uhifadhi kwa kiwango cha juu na kuwarudisha nyumbani kufanya kazi.
Mwenyekiti wa Karimjee Jivanjee Foundation, Yusuf Karimjee, amesema wazo la mpango huu lilianza porini, wakati marehemu Hatim Karimjee na Marcus Borner wa Frankfurt Zoological Society walipokuwa wakijadili jinsi ya kulinda mandhari waliyoyapenda.
Amesema hitimisho lao lilikuwa rahisi: watu waliopo katika nafasi nzuri zaidi ya kulinda mifumo ya ikolojia ya Tanzania ni Watanzania wenyewe.
“Mwaka 2016, imani hiyo ikawa ufadhili wa masomo – kutafuta vijana wenye vipaji vya uhifadhi, kuwapa mafunzo ya kiwango cha kimataifa, na kuwarudisha nyumbani.
“Mpango huo unawapeleka wanafunzi kusoma Shahada ya Uzamili (MSc) katika Usimamizi wa Uhifadhi wa Mifumo ya Ikolojia ya Kiafrika, kozi inayotolewa na Chuo Kikuu cha Glasgow.
“Wanafunzi hutumia mwaka mmoja kusoma Glasgow na mwaka wa pili katika mafunzo ya vitendo nchini Tanzania, yakiwemo mradi mrefu wa utafiti. Foundation inalipia ada zote na posho ya kujikimu, na inatoa hadi ufadhili mbili kila mwaka,” amesema.
Amesema mwaka wa pili wa vitendo uliongezwa kwa ushirikiano na Glasgow ili wanafunzi warudi wakiwa tayari kufanya kazi.

“Miaka kumi iliyopita, Tanzania haikuwa na mfumo thabiti wa wanasayansi wake wa uhifadhi waliofundishwa kwa kiwango hiki,” alisema Yusuf Karimjee na kuongeza: “Sasa tunao, na wengi wao wako humu ndani.
“Kwa miaka kumi, Watanzania 25, wa zamani na wa sasa, wamepitia ufadhili huu wa Glasgow. Kila mwanafunzi aliyemaliza mpango huo sasa anafanya kazi ya uhifadhi nchini Tanzania. 11 wameendelea na masomo ya PhD, na kwa pamoja wameandika karatasi 16 za kisayansi na kutoa mawasilisho zaidi ya 20 kwenye mikutano.
“Wanafunzi wetu wanaona ufadhili huu kama heshima kubwa, na hawaiisahau kamwe,” alisema Yusuf Karimjee.
“Wanahisi wajibu unaokuja nao, na wanaubeba. Kwa kila mhitimu, na kwa wanafunzi bado wako kwenye mpango: tunajivunia ninyi. Ninyi ndio moyo wa mpango huu.
“Nchi nzima, wahitimu wanafundisha wanasayansi wa uhifadhi na kuchangia utafiti unaosaidia usimamizi wa wanyamapori na usalama wa jamii,” amesema.
Amewahimiza wahitimu, wadau na wafanyakazi wa chuo kuungana na kufanya majadiliano ambayo yanaweza kuunda miaka 10 ijayo.



