Uwekezaji bil 290/- Savanna wazalisha ajira 2,100

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya Savanna Telecom (Africa) Limited imewekeza zaidi ya Sh bilioni 290 katika sekta ya mawasiliano nchini Tanzania, Uganda na Kenya, huku uwekezaji huo ukiambatana na upanuzi wa miundombinu na ongezeko la ajira katika nchi hizo.

Kampuni hiyo, inayoendesha huduma za intaneti kupitia mtandao wa Savanna Fibre, imeeleza kuwa tangu ilipoanza shughuli zake Februari 2024 ikiwa na wafanyakazi watatu, imefikia zaidi ya wafanyakazi 2,100 wa moja kwa moja na wa mikataba.

Takwimu zilizotolewa na kampuni hiyo wakati wa mkutano wa Africa Tech Festival unaofanyika Cape Town, Afrika Kusini, zinaonyesha kuwa ina zaidi ya kilomita 16,000 za miundombinu ya fibre katika nchi hizo, huku kilomita nyingine 8,000 zikiwa katika hatua za ujenzi.

Katika soko la Tanzania, kampuni hiyo inashikilia asilimia 41 ya huduma za intaneti ya kasi majumbani, huku nchini Uganda ikiwa na asilimia 56 ya soko hilo.

Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Rashmi Shah, alisema upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano unalenga kuongeza upatikanaji wa intaneti katika maeneo mbalimbali, ikiwemo miji midogo na vitongoji.

Alisema upatikanaji wa intaneti ni muhimu katika shughuli za kijamii na kiuchumi, zikiwemo elimu, biashara na huduma za afya.

Kwa sasa, kampuni hiyo ina zaidi ya wateja hai 250,000 na miundombinu inayofikia zaidi ya nyumba milioni moja.

Katika mpango wa upanuzi, kampuni imekamilisha usanifu wa kihandisi wa miundombinu inayolenga kufikisha huduma zake katika nyumba nyingine milioni moja ndani ya miezi 12 ya mwaka 2027.

Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano na kampuni ya teknolojia ya FiberHome.

Aidha, kampuni imeeleza kuwa wawekezaji wake wameongeza mtaji na kukamilisha taratibu za mikopo kwa ajili ya kufanikisha upanuzi huo, pamoja na maandalizi ya kuingia katika masoko mengine nje ya Afrika Mashariki.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button