Mabasi yagongana Chalinze, yajeruhi

PWANI; Watu watatu wamejeruhiwa baada ya mabasi mawili ya abiria kugongana leo Ijumaa, Novemba 20, 2026 majira ya asubuhi, katika eneo la Chamakweza, Chalinze, Barabara kuu ya Dar es Salaam – Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kennedy Mgani, amesema ajali hiyo imehusisha basi lenye namba za usajili T.453 DCX la Kampuni ya Saratoga, lililokuwa likiendeshwa na dereva Haji Ally (47), mkazi wa Kigoma, akitokea Kigoma kuelekea Dar es Salaam.
Amesema basi hilo liligongana na basi lenye namba za usajili T.331 DYL la Kampuni ya Ester, lililokuwa likiendeshwa na dereva John Kisingi (34), aliyekuwa akitokea Dar es Salaam kuelekea Arusha.
Amesema katika ajali hiyo, watu watatu waliokuwa kwenye basi la Saratoga wamepata majeraha. Majeruhi hao ni Mrina Mtambuka (33), mkazi wa Kibaha Mkoa wa Pwani, Haruna Yusufu (47), mkazi wa Kigoma, na Hamada Shabani (35), mkazi wa Kigoma ambaye ni kondakta wa basi la Saratoga.
Majeruhi wote wamepelekwa katika Kituo cha Afya Chalinze kwa matibabu zaidi na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi la Saratoga kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara.



