Upofu yamfungulia Jamila ‘scholarship’

IRINGA: CHANGAMOTO ya kupoteza uwezo wa kuona aliyokutana nayo Jamila Abdallah Nkomwa mwaka 2017, akiwa mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), haikumaliza ndoto zake za elimu, badala yake imekuwa mwanzo wa fursa mpya iliyomfungulia milango ya kuendelea na masomo na ajira.
Jamila, ambaye baada ya kukumbwa na changamoto hiyo alilazimika kusitisha masomo kwa miaka mitano, amepata ahadi ya kufadhiliwa masomo ya Shahada ya Uzamili na kuajiriwa baada ya kuhitimu, fursa aliyopewa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, katika Mahafali ya 18 ya MUCE yaliyofanyika mjini Iringa.
Ahadi hiyo imekuja baada ya Jamila kufanikiwa kurejea chuoni mwaka 2023, akiendelea na masomo kwa kutumia vifaa saidizi licha ya kutokuona, hadi kufikia hatua ya kuhitimu Shahada ya Awali ya Elimu katika Sayansi katika mahafali hayo.
Dk Kikwete, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alimpa Jamila fursa hiyo ya kuendeleza masomo yake katika ngazi ya uzamili na kumwahidi ajira baada ya kukamilisha masomo hayo, hatua itakayomwezesha kutumia taaluma yake kufundisha na kuwasaidia wanafunzi wengine.
Fursa hiyo ina maana kubwa kwa Jamila, ambaye kwa miaka kadhaa alikabiliwa na hali ngumu ya kutokuwa na uhakika wa kurejea katika masomo yake baada ya kupoteza uwezo wa kuona.

Akizungumza baada ya kupokea fursa hiyo, Jamila alisema ameipokea kwa furaha na kuahidi kuitumia vizuri kwa kusoma kwa bidii ili kuhakikisha anatimiza matarajio yaliyowekwa kwake.
Jamila alianza safari yake ya elimu ya juu mwaka 2016 alipojiunga na MUCE kusomea Shahada ya Awali ya Elimu katika Sayansi.
Hata hivyo, mwaka uliofuata, akiwa mwaka wa pili wa masomo na katika kipindi cha mafunzo kwa vitendo, alianza kupata matatizo makubwa ya macho yaliyosababisha kupoteza uwezo wa kuona.
Hali hiyo ilimlazimu kusitisha masomo yake wakati akiwa anakaribia kuanza mwaka wa tatu, huku familia yake ikianza jitihada za kutafuta matibabu katika hospitali mbalimbali kwa matumaini ya kurejesha uwezo wake wa kuona.
Baba yake, Abdala Mkomwa, alisema familia ilipitia kipindi kigumu huku ikitafuta msaada wa kitabibu katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Hospitali ya Mkoa wa Manyara iliyopo Babati, kabla ya kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Alisema pamoja na matibabu katika hospitali mbalimbali, familia ilijaribu pia tiba mbadala, ikitumaini binti yao angepona na kurejea katika hali yake ya kawaida.
“Tulihangaika huku na kule, tukampeleka hospitali mbalimbali na hata kujaribu tiba mbadala ili kuhakikisha anapona na kurejea katika hali yake ya kawaida. Tulianza Babati, baadaye tukapewa rufaa kwenda Muhimbili, lakini tuliambiwa kwamba Jamila asingeweza kurejeshewa uwezo wake wa kuona,” alisema.
Alisema taarifa hiyo iliwaumiza na kuwachanganya kama wazazi, hasa ikizingatiwa kuwa walikuwa na matumaini makubwa ya kuona binti yao akirejea katika masomo yake.
Hata hivyo, pamoja na changamoto hiyo, Jamila hakuruhusu hali yake kumaliza ndoto yake ya kupata elimu ya juu. Mwaka 2023 alirejea MUCE na kuendelea na masomo kwa kutumia vifaa saidizi vilivyomwezesha kujifunza na kushiriki katika shughuli za kitaaluma.
Hatimaye, juhudi hizo zimemwezesha kuhitimu shahada yake, huku mahafali ya 18 ya chuo hicho yakigeuka kuwa jukwaa la kupata fursa nyingine kubwa ya kuendeleza elimu na taaluma yake.
Kwa upande wake, Abdala alisema ahadi ya Dk. Kikwete imewapa furaha kubwa kama familia, kwa kuwa wameiona kuwa ni fursa muhimu inayompa binti yao nafasi ya kuendelea kujenga maisha yake kupitia elimu licha ya changamoto ya kutokuona.

Alisema baada ya miaka ya kuhangaika kutafuta matibabu na kukabiliana na hali ya binti yao, fursa hiyo imewapa matumaini mapya na kuwafanya waamini kuwa changamoto za maisha si mwisho wa safari ya mtu.
“Sisi kama wazazi leo hii tumeamini kwamba hakuna jambo lisilowezekana kwa Mwenyezi Mungu. Tumepokea vizuri sana kauli ya Rais Mstaafu na Mkuu wa Chuo. Kwa kweli furaha yetu imeongezeka, ni furaha isiyo na kifani,” alisema.
Kwa upande wake Jamila, alisema ahadi hiyo si msaada wa kuendeleza masomo pekee, bali pia ni nafasi ya kugeuza uzoefu wa changamoto alizopitia kuwa maarifa yatakayoweza kuwasaidia wengine.



