Waziri Mkuu kufanya ziara ya kikazi Moro

MOROGORO: WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, anatarajia kufanya ziara ya kikazi mkoani Morogoro kuanzia Novemba 21 hadi 26, mwaka huu, ambapo atafanya mikutano tisa ya hadhara kwa lengo la kuzungumza na wananchi, kusikiliza na kutatua kero zao pamoja na kukagua miradi ya maendeleo.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa ziara aliyoianza Mei mwaka huu, alipokutana na wananchi wa Wilaya ya Kilosa katika eneo la Dumila na Wilaya ya Gairo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Novemba 20, mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Sendiga, amesema ziara hiyo inalenga kumpa Waziri Mkuu fursa ya kukutana na wananchi wa maeneo mbalimbali ya mkoa huo na kusikiliza changamoto zinazowakabili.
Amesema Waziri Mkuu anatarajiwa kuwasili mkoani humo Novemba 21 na kuanza rasmi ziara yake Novemba 22, ambapo atatembelea wilaya sita ambazo ni Morogoro, Kilosa, Ulanga, Malinyi, Mvomero na Kilombero.

Sendiga amesema katika ziara hiyo, Waziri Mkuu atafanya mikutano tisa ya hadhara kwa lengo la kuzungumza na wananchi, kupokea kero zao, kuzitafutia ufumbuzi na kutoa maelekezo kwa mamlaka husika.
Aidha, amesema Waziri Mkuu atakagua miradi miwili ya maendeleo yenye thamani ya jumla ya Sh bilioni 49.7.
Amesema mradi wa kwanza ni wa Maji Miji 28 katika eneo la Kiburugutu, Halmashauri ya Mji Ifakara, wenye thamani ya Sh bilioni 48.
Mradi mwingine ni ujenzi wa Daraja la Isago, lenye thamani ya Sh bilioni 1.7, unaotekelezwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika Halmashauri ya Mlimba, Wilaya ya Kilombero.
Akizungumzia maandalizi ya ziara hiyo, Sendiga amewataka wananchi, watumishi wa umma, viongozi wa Serikali na vyama vyote vya siasa kujitokeza kwa wingi kushiriki mikutano hiyo na kumpokea Waziri Mkuu.
Pia, amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa huo, kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya pamoja na makatibu tawala wa wilaya, kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote atakayofanya mikutano ya hadhara.



