ESAMI: Afrika haipaswi kutegemea maarifa, teknolojia za nje

ARUSHA: TAASISI ya Usimamizi ya Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI) imetoa wito kwa nchi za Afrika kuongeza uwekezaji katika tafiti na ubunifu, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za utafiti na sekta binafsi ili matokeo ya tafiti yageuzwe kuwa bidhaa, teknolojia na huduma zinazochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Wito huo umetolewa wakati wa Kongamano la Pili la Kimataifa la Utafiti la ESAMI (ESAMI Global Research Colloquium 2026), lililofanyika jijini Arusha, ikiwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Kongamano hilo lenye kaulimbiu Ufadhili wa Utafiti Barani Afrika: Mifumo ya Utafiti, Ushirikiano, Miundombinu, Akili Mnemba na Uwekezaji wa Kibiashara katika Matokeo ya Tafiti, limewakutanisha watafiti, wasomi, watunga sera, viongozi wa taasisi, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kutoka maeneo mbalimbali.

Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo, Mkurugenzi wa Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu wa Usimamizi wa ESAMI, Dk. Henry Waruhiu, amesema Afrika haina upungufu wa wataalamu na watu wenye uwezo wa kufanya tafiti, bali changamoto kubwa ni ukosefu wa mifumo imara ya ufadhili na ushirikiano inayowezesha matokeo ya tafiti kutumika katika maisha halisi.
Amesema tafiti nyingi zenye ubora zimekuwa zikishia katika maktaba na machapisho ya kitaaluma badala ya kutumika kuboresha maisha ya wananchi, kuendeleza viwanda na kusaidia utungaji wa sera.
Dk. Waruhiu amesema kongamano la mwaka 2025 lililowakutanisha zaidi ya washiriki 500 kutoka taasisi 140 lilijadili mifumo ya utafiti barani Afrika, utawala wake, matokeo na athari zake kwa jamii.
Kuhusu miundombinu, amesema ni muhimu kuwekeza katika maabara, mifumo ya kuhifadhi takwimu na teknolojia za kidijitali ili kuwawezesha watafiti wa Afrika kushindana katika kiwango cha kimataifa.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ESAMI, Profesa David Kalaba, amesema utafiti unapaswa kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na changamoto zinazowakabili viongozi, serikali na sekta binafsi.
Amesema utafiti haupaswi kuishia kuwa shughuli ya kitaaluma pekee, bali unapaswa kusaidia kuboresha maamuzi na kuleta mabadiliko katika maisha ya wananchi.
Profesa Kalaba amesema ESAMI inahitaji kuunganisha mafunzo ya uongozi inayoyatoa na tafiti zinazofanyika ili kuhakikisha maarifa yanayozalishwa yanatumika kutatua changamoto za kiutendaji.
Akizungumza katika ufunguzi rasmi wa kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu wa ESAMI, Profesa Peter Kiruku, amesema Afrika inapaswa kujenga uwezo wake wa kuzalisha maarifa na teknolojia badala ya kuendelea kutegemea bidhaa na mifumo inayoagizwa kutoka nje.
Amesema dunia inapitia mabadiliko makubwa ya kiuchumi yanayochochewa na ushindani wa mataifa, mabadiliko ya mifumo ya uzalishaji na usambazaji wa bidhaa, mabadiliko ya tabianchi pamoja na maendeleo ya kasi ya teknolojia ya Akili Mnemba.
Profesa Kiruku amesema katika karne ya 20, utajiri wa mataifa ulipimwa kwa kiasi kikubwa kupitia rasilimali zilizokuwa chini ya ardhi, lakini katika karne ya 21 utajiri wa mataifa unazidi kutegemea maarifa yanayozalishwa katika maabara, vyuo vikuu, taasisi za tafiti za sera na vituo vya teknolojia.
“Hakuna bara linaloweza kuagiza uhuru wake wa viwanda kutoka nje. Huwezi kukabidhi wengine jukumu la kufikiri kwa niaba yako kisha ukatarajia kuwa na uwezo wa kuamua mustakabali wako,” alisema.



