Posta yatakiwa kuimarisha huduma kidijitali

DAR ES SALAAM. Serikali imelielekeza Shirika la Posta Tanzania kutumia vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) vilivyokabidhiwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuboresha mifumo ya utoaji huduma na kuongeza ufanisi katika kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya uchumi wa kidijitali.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Switbert Mkama, amesema mashirika ya posta duniani yanabadilika kutoka katika utoaji wa huduma za usafirishaji wa barua pekee na kuwa vituo vya huduma za kidijitali, biashara mtandao, ujumuishaji wa kifedha na huduma za Serikali mtandao.

Amesema mabadiliko hayo yanaonesha umuhimu wa Shirika la Posta Tanzania kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma ili kuendana na mahitaji ya sasa ya wananchi na uchumi wa kidijitali.
Aidha, amesema uwekezaji katika vifaa vya TEHAMA ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi wa kisasa na shindani unaotegemea maarifa, ubunifu na teknolojia, sambamba na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuimarisha uchumi wa kidijitali.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa UCSAF, Mlembwa Mnakua, amesema katika kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2023 hadi mwaka wa fedha uliopita, mfuko huo umewezesha ununuzi wa vifaa kwa ajili ya Shirika la Posta Tanzania vyenye thamani ya Sh bilioni 2.5.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, UCSAF imetenga Sh bilioni 1.8 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya TEHAMA pamoja na kuanzisha vituo vipya vya kutolea huduma za posta, hatua inayolenga kusogeza huduma hizo karibu zaidi na wananchi.

Kwa upande wake, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo, amesema shirika hilo limejipanga kuhakikisha vifaa vilivyokabidhiwa vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kuwanufaisha wananchi, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini.




