Dk Sajad atunukiwa tuzo mchango sekta ya mafuta

DAR ES SALAAM: MENEJA Mkazi wa Mansoor Industries, Dk Sajad Habib Rai, ametunukiwa tuzo na Mikono kwa kutambua mchango wake katika sekta ya nishati ya mafuta nchini.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo katika Mkutano wa Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi (CEO Summit) uliofanyika jijini Dar es Salaam, Novemba 26, 2026, Dk Sajad ameipongeza Serikali kwa kuendelea kusimamia sekta ya mafuta na kuweka mazingira yanayosaidia kudhibiti changamoto katika uagizaji na ununuzi wa mafuta.
Dk Sajad, ambaye amehusishwa na ubunifu wa mfumo wa udhibiti wa mafuta (BIL), amesema mchango wake katika kubuni mfumo huo ulilenga kukabiliana na udanganyifu katika uagizaji na ununuzi wa mafuta, hatua aliyosema imekuwa na manufaa kwa taifa.

“Kikubwa kwangu siku zote nikiwa kama mtaalamu katika sekta hii ya nishati ya mafuta huwa napenda kuona nchi yangu ikipiga hatua. Niliona kuna changamoto ya wizi wa mafuta wakati wa uagizaji na ununuzi, jambo lililonifanya kubuni kitu ambacho leo kimeliletea taifa faida,” amesema Dk Sajad.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha nchi inakabiliana na changamoto za kiuchumi, ikiwemo athari zinazotokana na migogoro ya kimataifa, huku akitaja mgogoro kati ya Marekani na Iran.
Awali, Mratibu wa CEO Summit, Deogratius Kihwele, amesema mkutano huo uliowakutanisha wakurugenzi wa taasisi mbalimbali, wawekezaji na watunga sera barani Afrika, ulilenga kujadili namna ya kuimarisha usalama wa uwekezaji, kulinda miundombinu na kuweka mikakati ya kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kuathiri watu, mali na shughuli za kiuchumi.
Washiriki wa mkutano huo walijadili namna taasisi na kampuni zinavyoweza kutambua usalama kama uwekezaji muhimu badala ya gharama za uendeshaji, wakieleza kuwa mifumo imara ya usalama inaweza kusaidia upanuzi wa biashara, kuongeza imani ya wawekezaji na kuimarisha ukuaji endelevu wa uchumi.

Mjadala mwingine uliangazia ulinzi wa wafanyakazi, wakandarasi na viongozi wa kampuni wanaofanya kazi katika mazingira yenye changamoto za kiusalama, hususan katika sekta za madini, usafirishaji na maendeleo ya miundombinu.
Katika eneo la miundombinu muhimu, washiriki walisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, waendeshaji wa miundombinu na kampuni binafsi za ulinzi katika kulinda vituo vya nishati, bandari, mitandao ya mawasiliano na mabomba dhidi ya wizi, hujuma na mashambulizi ya kimtandao.
Pia, usalama wa mifumo ya kidijitali ulikuwa miongoni mwa mada zilizojadiliwa, huku kampuni zikihimizwa kuimarisha uwezo wa kitaalamu, kuandaa mipango ya kukabiliana na mashambulizi ya kimtandao na kuweka mifumo ya kukabiliana na majanga yanayoweza kuathiri shughuli zao.



