Ukatili Watoto, wanawake watikisa Kagera

KAGERA: Matukio 205 ya ubakaji yameripotiwa mkoani Kagera katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2026, huku vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake vikiendelea kuwa changamoto licha ya juhudi za Jeshi la Polisi kupambana na uhalifu huo.
Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Charles Mimata, amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili, akieleza kuwa ubakaji unaendelea kuathiri watoto na wanawake katika jamii.
Amesema matukio mengine yanayotikisa mkoa huo ni ulawiti wa watoto na mauaji, ambayo yamekuwa yakichochea maumivu, chuki na visasi katika jamii.

Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi, Wilaya ya Bukoba inaongoza kwa matukio ya ukatili yaliyoripotiwa, ikiwa na matukio 60, yakiwemo ubakaji 51, ulawiti sita, mauaji ya mtoto mmoja na mauaji ya wanawake mawili. Wilaya ya Karagwe imeripoti matukio 48, Missenyi 38, Muleba 31 na Biharamulo 15.
Mimata amesema katika kipindi hicho kesi 54 za mauaji zilizofikishwa mahakamani, watuhumiwa 18 wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa na 36 wamehukumiwa kifungo cha maisha. Kesi 10 za ulawiti, watuhumiwa wanane wamehukumiwa kifungo cha maisha na wawili kunyongwa hadi kufa, huku katika kesi 65 za ubakaji, watuhumiwa 16 wamehukumiwa kifungo cha maisha na 49 kifungo cha miaka 30 jela.

Amesema kesi nyingine zinaendelea katika hatua mbalimbali za kisheria, ikiwemo uchunguzi na upatikanaji wa mashahidi, huku Jeshi la Polisi likiendelea kushirikiana na taasisi za serikali na zisizo za serikali katika kutoa elimu na kukabiliana na ukatili.
Katika kuimarisha uelewa wa jamii, amesema zaidi ya mikutano 960 imefanyika kupitia wakaguzi wa kata kuanzia Januari hadi Novemba 2026, huku Dawati la Jinsia na Watoto likiimarishwa na wananchi wakihamasishwa kutoa taarifa kupitia namba 0699 913 200 inayopatikana saa 24 bila malipo.

Takwimu za Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa ubakaji umepungua kutoka matukio 221 mwaka 2025 hadi 205 mwaka 2026, wakati ulawiti umeongezeka kutoka 12 hadi 16 na mauaji ya watoto kutoka tisa hadi 10. Mauaji ya wanawake yamepungua kutoka 42 hadi 19 katika kipindi hicho.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukoba, Proscovia Jakamwambi, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya jamii, taasisi za serikali na wadau mbalimbali katika kupinga ukatili na kulinda haki za wanawake na watoto.

Ameitaka Jeshi la Polisi kuongeza ulinzi kwa wanawake na watoto, huku akihimiza jamii kutowaficha wanaotenda vitendo vya ulawiti na ukatili hata kama ni watu wa karibu au ndugu wa familia, ili kusaidia kukomesha vitendo hivyo.
Jakamwambi amesema kampeni hiyo inalenga kuhamasisha jamii kutambua, kuzuia na kuripoti vitendo vya ukatili, akieleza kuwa vitendo hivyo vinahatarisha usalama, vinaweza kuongeza umasikini na kuchochea chuki katika jamii.




NEW88 – Sân chơi giải trí hàng đầu với nhiều chương trình khuyến mãi hấp dẫn tham gia tại website: https://apu.com.tw/