‘Tanroads izingatie utu ubomoaji’

KIGOMA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Kigoma kuzingatia utu na ubinadamu wakati wa kuwaondoa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao kandokando ya barabara, akisema utekelezaji usiozingatia hali za wananchi unaweza kuongeza umaskini na chuki dhidi ya Serikali.

Profesa Mkumbo ametoa kauli hiyo katika kongamano la siku moja na wafanyabiashara na wawekezaji wa Mkoa wa Kigoma, baada ya kupokea malalamiko ya wafanyabiashara walioondolewa katika maeneo yao ya biashara, huku baadhi wakidai bidhaa zao bado zipo ndani ya mabanda yaliyobomolewa na hawana maeneo mbadala ya kuendeleza shughuli zao.

Amesema amepokea simu kutoka mikoa mbalimbali, ikiwemo kwa wafanyabiashara na viongozi wa Jimbo la Ubungo, Dar es Salaam, wakilalamikia kubomolewa kwa mabanda yao na kuondolewa katika maeneo waliyokuwa wakitegemea kuendesha familia zao.

Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini, Revocatus Chipando (Baba Levo) (wa pili kulia) akizungumza mbele ya Waziri Mkumbo kuhusu bomoa bomoa inayofanywa na TANROADS

“Tunajua zipo sheria na kanuni ambazo zimetumika kutekeleza jambo hilo, lakini pia kuna wakati utu na ubinadamu lazima uangaliwe, kwani wananchi hao ni Watanzania na Serikali inawategemea kwa mambo mbalimbali. Suala hilo lisitekelezwe katika hali ambayo itawaumiza wengine na kuwafanya wafanyabiashara hao kujenga chuki na Serikali,” amesema.

Awali, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga Mkoa wa Kigoma (SHIUMA), Moran Mgina, amesema wafanyabiashara waliomba kupewa muda wa kuhamisha bidhaa zao, lakini watendaji wa TANROADS kwa kushirikiana na mgambo wa Manispaa na polisi kutoka Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Kigoma wameendelea na ubomoaji bila kusikiliza maombi na ushauri wao.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, Revocatus Chipando maarufu Baba Levo, amesema amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu zoezi hilo, akieleza kuwa baadhi yao walikuwa tayari kulipa ili waendelee kutumia maeneo hayo, lakini TANROADS iliwataka kuondoka kwanza na kusubiri maelekezo mengine baadaye.

Akijibu hoja hizo, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Mwita Joram, amesema wakala huo umefuata sheria na taratibu zote katika kutekeleza zoezi hilo, ikiwemo kutoa notisi tangu mwaka jana, lakini wafanyabiashara wengi hawakuzingatia maelekezo yaliyotolewa.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button