Wananchi Naisinyai wasogezewa tanki la maji

ARUSHA: Wananchi wa Kijiji cha Naisinyai, Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara, wanatarajiwa kupunguza adha ya kutafuta maji nyakati za usiku na alfajiri baada ya Kampuni ya Franone Mining & Gems kuwapatia tanki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 10,000.

Tanki hilo lenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 3.5 limetolewa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Wajibu kwa Jamii (CSR) wa kampuni hiyo inayochimba madini ya Tanzanite kwa ubia na Serikali katika Kitalu C, Mirerani.

Hatua hiyo inalenga kuwasaidia wananchi, hususan wanawake na watoto ambao wamekuwa wakihangaika kutafuta maji nyakati za usiku na alfajiri kutokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo kijijini hapo.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Mwenyekiti wa Kijiji cha Naisinyai, Joseph Maliaki Laizer, ameishukuru kampuni hiyo kwa kuwezesha upatikanaji wa tanki hilo pamoja na kuandaa eneo maalumu la kunyweshea mifugo na huduma ya maji kwa wananchi wa eneo la Samax.

Amesema msaada huo ni muhimu kwa jamii kwa kuwa maji yanapatikana kwa matumizi ya wananchi na wafugaji bila malipo.

“Tunamshukuru Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining & Gems, Onesmo Mbise, kwa kutupatia tenki hilo na maji hayo ambayo wafugaji wanayatumia kunyweshea mifugo na jamii inatumia bila kulipia fedha yoyote,” alisema Laizer.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Naisinyai, Patimayo Mollel, akisoma taarifa ya wananchi, amesema jamii inatoa shukrani kwa kampuni hiyo kwa kuwezesha huduma ya maji inayowanufaisha wakazi wa eneo hilo.

“Tunaishukuru kampuni ya Franone kwa kutupatia tawi la maji linalotumika kunyweshea mifugo na vitalu viwili vya maji katika eneo la Samax kwa ajili ya wananchi wanaoishi eneo hilo,” alisema Mollel.

Naye Diwani wa Kata ya Naisinyai, Taiko Kurian Laizer, ameishukuru Franone Mining & Gems Ltd kwa misaada inayotolewa kwa jamii inayozunguka mgodi wa Kitalu C, huku akiwataka wachimbaji wengine kuiga mfano huo wa kushirikiana na wananchi.

“Kila mara Franone Mining & Gems Ltd mmekuwa mstari wa mbele kuwezesha CSR kwa jamii inayowazunguka, hivyo wachimbaji wengine waige mfano wenu,” alisema diwani huyo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Onesmo Mbise, Meneja wa Mgodi, Frank Mziwanda, amesema tanki hilo lina uwezo wa kuhifadhi lita 10,000 za maji na thamani yake ni Sh milioni tatu.

Amesema kampuni itaendelea kushirikiana na wananchi wa kijiji hicho katika kuboresha huduma za kijamii ikiwemo maji, afya, elimu na barabara, kwa lengo la kuhakikisha jamii inanufaika na matunda ya madini ya Tanzanite yanayozalishwa katika Kitalu C.

“Mkurugenzi wa kampuni amenieleza niwaambie kuwa milango ya kampuni ipo wazi. Endapo kuna jambo la kufikisha kwa uongozi, mnakaribishwa,” alisema Mziwanda.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button