Serikali yaonya madereva wasiofuata sheria

DAR ES SALAAM: SERIKALI imewataka wamiliki wa vyombo vya moto kufuata sheria za barabarani ili waweze kuepukana na ajali zinazoweza kuzuwilika huku ikisistiza watakao kwenda kinyume na onyo hilo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha imezitaka mamlaka zinazohusika na usalama barabarani kuchukua hatua dhidi ya madereva wazembe, ikieleza kuwa tabia zao zinahatarisha maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara, huku zikisababisha hasara kwa familia na taifa.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, wakati akifungua Kongamano la Usalama Barabarani Afrika 2026 lililoandaliwa na Taasisi ya Mpango wa Usalama Barabarani (TARSI) jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuwakutanisha wadau kujadili namna ya kupunguza ajali.

Kihenzile amesema ajali za barabarani zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito kwa sababu madhara yake hayaishii kwenye vifo na majeraha, bali pia huacha familia katika majonzi, watoto yatima na taifa kupoteza nguvu kazi inayochangia maendeleo.

Amewataka washiriki wa kongamano hilo kuchunguza sababu za ajali, ikiwemo kama adhabu zilizopo zinatosha, mifumo ya usimamizi inafanya kazi ipasavyo, miundombinu ina changamoto na kama usimamizi wa madereva unatekelezwa kwa ufanisi.

Amesema ni muhimu kujiuliza dereva anajisikiaje anapohatarisha maisha ya abiria 60 waliopanda gari kwa lengo la kwenda kutafuta riziki na kusaidia familia zao, lakini kutokana na uzembe wake baadhi yao wanapoteza maisha au kupata ulemavu.

Kihenzile amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika barabara, madaraja, bandari na viwanja vya ndege, lakini mafanikio ya miundombinu hiyo hayapaswi kupimwa kwa uwezo wa kusafirisha watu na mizigo kwa haraka pekee, bali pia kuhakikisha wanafika salama.

Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara, kuweka mifumo ya kudhibiti maeneo yenye ajali nyingi na kuchukua hatua dhidi ya madereva wanaokiuka sheria.

Ameitaja Jeshi la Polisi kuwa na wajibu wa kuwawajibisha madereva wanaoendesha magari kwa uzembe, akieleza kuwa vitendo vyao vinaweza kuathiri maisha ya watu wengi wasio na hatia.

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mhandisi Rogatus Mativila amesema usalama barabarani unahitaji ushirikiano wa Serikali na wadau mbalimbali kwa kuwa ajali zinaondoa nguvu kazi ya taifa na kuacha watu wakiwa na majeraha na ulemavu.

Amesema ingawa kwa mtazamo wake ajali kubwa zilizokuwa zikitokea miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000 zimepungua, bado juhudi zinahitajika kuhakikisha hali ya usalama barabarani inaendelea kuimarika.

Ametolea mfano wa kipindi ambacho ajali za mabasi zilikuwa zikitokea mara kwa mara na kusababisha vifo vya watu wengi, hali iliyosababisha Serikali kuweka zuio la mabasi kusafiri usiku.

Amesema baadaye Serikali na Jeshi la Polisi ziliimarisha udhibiti, ikiwemo matumizi ya vidhibiti mwendo na hatua nyingine za usalama, na kuruhusu tena mabasi kusafiri usiku.

Hata hivyo, amesema elimu kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara inapaswa kuendelea, akitaja baadhi ya madereva wanaoendesha kwa mwendokasi katika maeneo ya makazi ambako kikomo ni kilomita 50 kwa saa.

Amesema wapo wanaofika mwendo wa kilomita 100, 160 hadi 200 kwa saa katika maeneo hayo, jambo linaloweka maisha ya watu hatarini.

Ameongeza kuwa usalama barabarani hauwahusu madereva pekee, bali pia wahandisi na wajenzi wa miundombinu ambao wanapaswa kuzingatia usalama kuanzia hatua za usanifu hadi ujenzi wa barabara.

Akieleza uzoefu wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Ardhi na TEHAMA ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Mwakilishi wa Mwera, Mihayo Juma N’hunga, amesema wameanza kutumia teknolojia ya kamera za CCTV katika barabara kuu na maeneo mbalimbali ya kuingia mjini kudhibiti makosa ya barabarani.

Amesema kamera hizo zimeunganishwa na mfumo wa usajili wa namba za magari na taarifa za wamiliki, hivyo dereva anapokiuka sheria anaweza kutumiwa ujumbe mfupi wa simu ndani ya dakika tano ukimweleza kosa alilofanya.

Ametaja makosa yanayoweza kubainika kupitia mfumo huo kuwa ni mwendokasi, kutofunga mkanda na kutumia simu wakati wa kuendesha gari.

N’hunga amesema lengo la matumizi ya teknolojia hiyo si kuongeza mapato ya Serikali kupitia faini, bali kuwasaidia madereva kuzingatia sheria na kuendesha katika mazingira salama.

“Lengo siyo kwenda kukusanya mapato, lengo ni kusaidia madereva wanapokuwa wanaendesha wawe katika mazingira ya usalama,” amesema.

Amesema katika kipindi cha takribani miezi sita tangu hatua hizo kuanza kutekelezwa, ajali zisizo za lazima katika maeneo ya mjini zimepungua kwa kiwango kikubwa, akitaja uwekezaji wa Serikali ya Zanzibar katika ujenzi na matengenezo ya barabara kuwa sehemu ya juhudi hizo.

Ameeleza kuwa uzoefu huo unaweza kushirikishwa na wadau wengine ili kusaidia maeneo yanayokabiliwa na changamoto za ajali, huku akitaka uchunguzi ufanyike katika maeneo yanayotokea ajali mara kwa mara ili kubaini kama kuna kasoro za miundombinu au alama za barabarani zinazohitaji kurekebishwa.

Akizungumzia sababu za kuandaa kongamano hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa TARSI, Maliki Barongo, amesema wamekusudia kuwakutanisha wadau wa makundi mbalimbali ili kujadili kwa pamoja namna ya kupunguza ajali za barabarani.

Amesema wadau hao ni pamoja na madereva, watembea kwa miguu, wahandisi, wajenzi wa miundombinu, kamati za miundombinu, Jeshi la Polisi na wataalamu wa afya.

Barongo amesema elimu ya usalama barabarani haipaswi kuelekezwa kwa madereva pekee, bali pia kwa wahandisi na wajenzi wanaosanifu na kujenga barabara ili wahakikishe usalama unazingatiwa kuanzia hatua za usanifu hadi utekelezaji wa miradi.

Amesema ajali zinapotokea, pamoja na kupoteza maisha na kusababisha ulemavu wa kudumu, pia huathiri uchumi wa taifa kutokana na kupotea kwa nguvu kazi na kuharibika kwa miundombinu ambayo Serikali hutumia fedha nyingi kuijenga na kuitengeneza.

Amesema kupitia kongamano hilo, wadau watabadilishana uzoefu na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali kuhusu mbinu zinazotumika kupunguza ajali, kisha kuandaa mapendekezo yatakayowasilishwa Serikalini kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Barongo amesema TARSI inaamini ushirikiano huo utasaidia kuishauri Serikali na jamii kwa ujumla kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa kupunguza ajali na kuimarisha usalama wa watumiaji wote wa barabara.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button