TRAPCA yaimarisha uwezo wa Afrika biashara kimataifa

ARUSHA: KITUO cha Mafunzo ya Sera za Biashara (TRAPCA) kimetajwa kuwa na mchango mkubwa katika kujenga uwezo wa wataalamu wa Afrika kwenye masuala ya biashara na sheria zake, hatua inayosaidia nchi za bara hilo kushiriki kikamilifu katika mfumo wa biashara ya kimataifa.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Usimamizi ya Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI), Profesa Peter Kioloku, amesema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya TRAPCA yaliyofanyika jijini Arusha jana, akieleza kuwa kituo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo kwa wataalamu kutoka nchi mbalimbali za Afrika tangu kilipoanzishwa.

Amesema katika kipindi hicho, TRAPCA imetoa mafunzo kuanzia ngazi ya cheti hadi Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Sera za Biashara ya Kimataifa na Sheria za Biashara, ikiwa na lengo la kuongeza utaalamu na kuwawezesha wataalamu wa Afrika kusimamia maslahi ya nchi zao katika majadiliano ya biashara.

Alieleza kuwa kituo hicho kilianzishwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden ili kuongeza uwezo wa kitaalamu katika masuala ya biashara barani Afrika.

Kwa upande wake, Mkuu wa TRAPCA, Profesa Kefa Chekoti, amesema kituo hicho kitaendelea kushirikiana na serikali za Afrika katika kujenga uwezo wa wataalamu ili kuwezesha utekelezaji wa makubaliano ya biashara yaliyosainiwa na nchi mbalimbali.

Amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 20, bado kuna changamoto ya kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kwa ufanisi, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa umma, sekta binafsi na asasi za kiraia.

Ameongeza kuwa ESAMI na TRAPCA ziko tayari kusaidia serikali kuziba mapengo ya kitaalamu kwa kutoa uelewa kuhusu namna makubaliano ya biashara yanavyofanya kazi na mchango wake katika kukuza uchumi wa nchi.

Profesa Chekoti amesema wahitimu wa TRAPCA sasa wanashika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini na katika jumuiya za kikanda, zikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), COMESA, ECOWAS na IGAD.

Wengine wanahudumu katika taasisi za kimataifa zikiwemo Shirika la Biashara Duniani (WTO), Benki ya Dunia, Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD), Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) na Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button