Vodacom yaja na zawadi msimu wa sikukuu

DAR ES SALAAM: Msimu wa sikukuu unaoambatana na ongezeko la manunuzi, safari na shughuli za kijamii umeendelea kuchochea matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali, huku wateja wakipata fursa ya kufanya miamala bila kutegemea fedha taslimu na kushiriki katika kampeni mbalimbali za zawadi.
Katika kuhamasisha mabadiliko hayo, Vodacom Tanzania imezindua kampeni ya wiki nane kupitia huduma ya M-Pesa yenye kaulimbiu ‘Zaidi ya Malipo, Ni Shangwe’, inayowapa wateja wanaokidhi vigezo nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali, zikiwemo magari matano aina ya Jetour T2, vikapu 600 vya sikukuu na marejesho ya hadi asilimia 10 ya fedha kwa baadhi ya malipo.
Kampeni hiyo iliyozinduliwa Novemba 27, 2026, inalenga kuhamasisha matumizi ya malipo ya simu katika shughuli za kila siku, wakati kipindi cha sikukuu kikitarajiwa kuhusisha matumizi zaidi katika manunuzi, usafiri, migahawa na huduma nyingine.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, amesema matumizi ya malipo ya simu yanaweza kusaidia kupunguza changamoto zinazohusiana na kubeba fedha taslimu, ikiwemo hatari ya kupoteza fedha, kupata chenji na kutumia muda mwingi kwenye foleni.
Amesema kupitia M-Pesa, wananchi wanaweza kufanya malipo ya bidhaa na huduma mbalimbali, ikiwemo kujaza mafuta, kufanya manunuzi na kulipia huduma wanazotumia wanapokuwa safarini au katika shughuli za kijamii.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa M-Pesa, Tulisindo Mlupilo, amesema kuhamasisha matumizi ya malipo ya kidijitali katika shughuli za kawaida ni sehemu ya kujenga mazoea ya kufanya miamala kwa njia zinazorahisisha maisha ya wateja na wafanyabiashara.
Kupitia kampeni hiyo, wateja wanaofanya malipo yanayokidhi vigezo na masharti watashiriki droo za zawadi zinazojumuisha magari matano, vikapu 600 vya sikukuu, simu janja za Samsung kwa wateja wa VYB, zawadi za papo hapo na punguzo la bei katika biashara zinazoshiriki.
Huduma ya M-Pesa inawawezesha wateja kufanya malipo kwa kutumia msimbo wa QR, Lipa Namba au M-Pesa Visa Card, pamoja na kulipia bili mbalimbali, kununua muda wa maongezi na vifurushi vya intaneti, tiketi za mabasi, treni ya SGR na baadhi ya huduma za ndege.
Vodacom imesema katika kipindi cha kampeni hiyo itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara na kufanya shughuli za uhamasishaji katika maeneo mbalimbali nchini, huku makabidhiano ya zawadi yakifanyika katika mikoa mbalimbali.



