Mwigulu: Tudumishe Utamaduni wa Kitanzania

WAZIRI MKUU, Dk. Mwigulu Nchemba ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) nchini kuzingatia maadili ya Kitanzania na uzalendo katika utekelezaji wa shughuli zao, huku akiyaonya dhidi ya kupokea fedha zenye masharti yanayoweza kuhatarisha utu na maadili ya Watanzania.
Aidha, ameyataka mashirika hayo kubuni vyanzo vipya vya mapato ndani ya nchi, kuimarisha ubia na kutumia ubunifu ili kuhakikisha huduma muhimu wanazozitoa kwa jamii haziathiriki kutokana na kupungua kwa ufadhili kutoka kwa wahisani. Waziri Mkuu ametoa wito huo wakati akifungua Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Amesisitiza umuhimu wa kulinda utu na maadili ya Watanzania, alisema mashirika hayo yanapaswa kuhakikisha fedha wanazopokea zinachangia maendeleo ya jamii badala ya kuwa na masharti yanayoweza kuathiri misingi ya Taifa.
“Tusipokee fedha za kutuangamiza. Tunatafuta fedha ili tulinde utu na tuboreshe ustawi wa Mtanzania, si kupata fedha zenye masharti yanayohatarisha maadili yetu, kizazi cha sasa na kijacho. Lazima tulinde utu wetu na mustakabali wa Taifa letu kwa gharama yoyote ile,” alisema.

Ameyapongeza mashirika hayo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma muhimu zikiwemo elimu, afya, maji na ustawi wa jamii, akisema mchango wake ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.
Aidha, ameyataka mashirika hayo kuoanisha mipango na shughuli zao na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano, akieleza kuwa utekelezaji wa Dira hiyo unahitaji ushiriki wa wadau wote. Amebainisha kuwa sekta binafsi inatarajiwa kuchangia asilimia 70 ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, alimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wa mwaka 2022/23 hadi 2026/27.
Amesema sekta hiyo imepiga hatua katika utoaji wa huduma, uzalishaji wa ajira na kuwafikia wananchi, huku akihimiza mashirika hayo kuendelea kutumia ubunifu, kuimarisha ubia na kutafuta vyanzo vya ndani vya fedha. SOMA: NGO’s Mtwara walalamikia upungufu wa wafadhili

Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Jasper Makala, alisema jukwaa hilo ni fursa kwa mashirika hayo kujipanga upya kwa kuimarisha vyanzo vya ndani vya mapato na kupunguza utegemezi wa ufadhili kutoka nje. Amesisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha uendelevu wa huduma kwa wananchi na kuimarisha mchango wa mashirika hayo katika maendeleo ya Taifa.



