Nchi nane zatajwa mabinti wanakotumikishwa kingono

SERIKALI imetaja nchi wanazodaiwa kupelekwa wasichana wa kitanzania kwenda kutumikishwa kingono.

Ofisa Mwandamizi  kutoka Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Ahmad Mwindadi  alitaja nchi hizo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahamaji Duniani.

Nchi hizo ni pamoja na Oman, India, Italia, Thailand, Indonesia, Uturuki, Iraq na Kenya huku watu wenye ulemavu pia wakidaiwa kusafirishwa kwa ajili ya kufanya kazi ya kuombaomba.

Alisema kwa sasa serikali inawasaka mawakala wanaowachukua wanawake  nchini na kuwapeleka ughaibuni bila kufuata taratibu za uhamiaji kisha kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwamo kutumikishwa kingono.

Imeelezwa kuwa mawakala hao wamekuwa wakiwarubuni wasichana kwamba wanakwenda kuwatafutia kazi zenye ujira mnono, hivyo kujikuta katika mateso.

Mwindadi alisema wahamaji wamekuwa wakitoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya kutafuta fursa za biashara, uwekezaji, kazi na wakati mwingine wanahama kwa sababu ya machafuko ya kisiasa.

“Wasichana wengi hapa nchini wamekuwa wakirubuniwa na mawakala kwamba wanawatafutia kazi nje ya nchi lakini hawafuati taratibu na sheria za uhamiaji, hivyo wanajikuta kwenye mateso,” alisema.

Alisisitiza kuwa wasichana na wanawake hao wanapofika kwenye nchi hizo, wamekuwa waathirika wa vitengo vya ukatili wa jinsia ikiwamo  kutumikishwa kingono.

Kuhusu watu wenye ulemavu, alisema wamekuwa na soko  nchini Kenya baada ya kusafirishwa kwa njia haramu kwa ajili ya kwenda kuombaomba.

“Watu wengi wanatafuta fursa katika nchi mbalimbali lakini tunawataka kufuata sheria za uhamiaji kwa sababu kutofuata utaratibu husababisha kukosa haki zao kama wahamaji. Tunaendelea kuwasaka na kupambana na mawakala hawa ili tuwachukulie hatua za kisheria,” alieleza.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Wahamaji (IOM), zaidi ya watu 17,000 ni waathirika wa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu waliotambuliwa katika nchi na maeneo 123.

Pia limebainisha wahalifu 37,000 waliofanikisha mchakato wa usafirishaji haramu wa binadamu kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2022.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini alisema kuwa wazazi na walezi wanapaswa kuwasimamia na kuwalinda vijana wao hususani mabinti wasirubuniwe na mawakala wenye nia ovu kwa ahadi ya kuwatafutia kazi.

Alisema kuwa mabinti hao wamekuwa waathirika wa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo kuteswa, kunyanyaswa, kutumikishwa kingono na kufanya kazi zisizo na staha.

“Wazazi na walezi tuwalinde mabinti zetu wasirubuniwe na mawakala hawa kwa sababu hawafuati sheria za uhamaji na nia zao ni ovu kwa sababu hawawatafuti kazi zenye staha kama wanavyoeleza,” alisema.

Alitaja changamoto mbalimbali wanazopitia wahamaji ni kutengwa, kubaguliwa, kuteswa na hata kufa kutokana na mazingira wanayoyakuta.

Sagini alisema wahamaji wanapaswa kutumiwa kama fursa ya kukuza uchumi kupitia uwekezaji, wataalamu wa kigeni katika sekta mbalimbali na utalii.

“Ukuaji wa teknolojia umekuwa sababu ya ongezeko la wahamaji kwani wanatafuta fursa mpya za kiuchumi, masomo, ajira na uwapo wa miundombinu ya usafiri bila kikwazo huongeza wahamaji. Tutaendelea kudhibiti wahamaji haramu ili wasihatarishe usalama wa nchi,” alisema.

Alifafanua kuwa wanaendelea na utaratibu wa usajili wa wageni walowezi walioishi nchini kwa muda mrefu ili watambulike na kupewa hadhi ya kuwa wakazi wa nchini.

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhamiaji nchini, Dk Anna Makakala alisema Januari hadi Novemba mwaka huu, jumla ya raia wa kigeni 1,172,205 waliingia nchini kwa madhumuni mbalimbali ikiwamo utalii, matembezi, masomo na shughuli nyingine za muda mfupi. Katika kipindi hicho, watu 983,189 walitoka nchini na waliorejea kutoka mataifa mbalimbali ni 220,423.

Alisema walitoa vibali vya ukazi vya kielektroniki 16,022 kwa raia wa kigeni, viza 500,711 na hati za kusafiria kwa Watanzania 110,137 kwa kipindi hicho.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button