Maandalizi mchakato wa katiba mpya yaiva 

VYAMA vya siasa na wananchi vimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aitishe kikao maalumu cha Baraza la Vyama vya Siasa.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus imeeleza kuwa lengo la kikao hicho alichoagiza Rais Samia ni kushirikisha wadau kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya kikosikazi kilichoratibu maoni kuhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Mohamed Ngulangwa alilieleza HabariLEO jana kwamba wanaunga mkono agizo la Rais Samia.

“La kwanza ni kumpongeza hii inaonesha ni kwa kiasi gani anayaishi maneno yake ambayo aliyatamka Julai mwaka jana na ameona wakati mwafaka ni sasa hivyo sisi hatuna hiyana tupo tayari kukutana na msajili wa vyama vya siasa na kujadiliana kwa maslahi mapana ya nchi yetu,” alisema Ngulangwa na kuongeza:

“Tujikite zaidi kwenye mapendekezo yale yaliyomo kwenye kikosi kazi, hata kama Katiba mpya itachelewa baada ya uchaguzi wa 2025”.

Katibu Mkuu wa Chama cha ADC, Doyo Hassan alimpongeza Rais Samia kwa jitihada za kukuza demokrasia nchini na kuahidi kumpa ushirikiano.

“Sisi tupo tayari kwa majadiliano na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini kwa kuwa Rais anatambua mchango wa vyama vingi nchini lakini mapendekezo yetu makubwa ni mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa,” alisema Doyo.

Chama cha ACT-Wazalendo kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu kilieleza kuwa kinaunga mkono agizo la Rais Samia.

“Ni matumaini yetu kuwa kikao hicho kitapatiwa ratiba hiyo itakayohakikisha tuna sheria mpya ya uchaguzi, sheria mpya ya vyama vya siasa kabla ya mwisho wa mwaka huu na kuhakikisha kwamba mabadiliko ya sheria ya mabadiliko ya katiba yanafanyika ili kuanza mchakato wa Katiba kwa kuundwa kwa timu ya wataalamu kama ilivyopendekezwa na kikosi kazi,” ilieleza Shaibu.

Wananchi wanena

Mkazi wa Kinondoni Mkwajuni mkoani Dar es Salaam, Alex Putto alisema Rais Samia ameonesha uzalendo kwa nchi yake na ataongeza mshikamano wa taifa kwa kutambua mchango wa vyama vingi vya siasa.

“Anastahili pongezi, ameonesha kukuza demokrasia na ushirikishwaji wa Watanzania katika masuala mbalimbali yanayolihusu taifa lao kama kitu kimoja kwa maslahi ya taifa,” alisema Putto.

Dunstan Mahimbo ambaye ni mkazi wa Kimara Korogwe mkoani Dar es Salaam alisema agizo la Rais Samia litaimarisha mshimamano wa Watanzania kwa kujiona ni wamoja.

Kwa mujibu wa taarifa ya Zuhura kwa vyombo vya habari, Rais Samia alitoa maelekezo hayo wakati wa kikao kilichofanyika Ikulu ya Chamwino, kilichohudhuriwa na viongozi wa serikali kuhusu kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya.

Zuhura alieleza kuwa kikao hicho kilijadili namna ya kushirikisha wadau na hasa ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato huo kutoka pande zote mbili Tanzania Bara na Zanzibar.

Alieleza kuwaq mbali na mchakato wa Katiba mpya, masuala mengine yanayotarajiwa kushughulikiwa ni marekebisho ya sheria zinazohusiana na uchaguzi zikiwemo Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Zuhura alieleza miongoni mwa viongozi waliohudhuria kikao hicho ni Waziri waNchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro na watendaji wa taasisi.

Hivi karibuni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro alilieza Bunge kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24 wizara hiyo imejipanga kutekeleza vipaumbele 30 kikiwamo cha kuratibu mchakato wa Katiba Mpya.

Dk Ndumbaro alisema hayo bungeni Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Awali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema katika mwaka wa fedha 2023/24 shughuli za maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka 2024 zitaendelea.

Majaliwa alisema hayo bungeni Dodoma wakati akiwasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/24.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button