Dk Mwinyi aziita kampuni za bima kwenye miradi
RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema serikali yake inayakaribisha mashirika ya bima yaende Zanzibar kuwekeza kwenye miradi.
Dk Mwinyi alisema hayo jana alipofungua mkutano wa 44 wa Umoja wa Wanabima Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika (OESAI).
Alisema wakati serikali inafanya mageuzi ya kiuchumi kuna haja ya sekta ya bima kuwepo kwenye eneo la uwekezaji ili kuwa na kinga katika fedha za miradi hiyo.
Pia, alisema kuna ongezeko la kampuni za bima hivyo kuna haja ya kujitanua kwenye uwekezaji wa miradi mikubwa ili kuunga mkono jitihada za mageuzi ya kiuchumi.
Dk Mwinyi alisema wakati Serikali inaendelea na utekelezaji wa sera ya uchumi wa buluu kwenye sekta ya mafuta na gesi, uvuvi, utalii na kilimo cha zao la mwani ni vema mashirika hayo ya bima kutumia fursa ya kuwekeza kwenye maeneo hayo.
Kamishna wa Bima Tanzania, Dk Baghayo Abdallah Saqware alisema sekta ya bima ni muhimu kwa kuwa inaongeza mzunguko wa rasilimali fedha na kutoa kinga kwa wananchi wakati wa majanga.



