Shule 4 sekondari zapewa kompyuta 100

SHULE nne katika mikoa ya Tanga na Pwani zimepata msaada wa kompyuta 100 zenye thamani ya Sh milioni 37, ili kuwezesha wanafunzi kupata masomo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Kupita msaada huo kila shule imepata kompyuta 25 zilizotolewa na Shirika la Camara Education Tanzania kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), ambayo ina jukumu la kisheria la kukusanya michango kwa ajili ya sekta ya elimu nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Jokate Mwegelo amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii kutoka na kuwekewa mazingira mazuri ya kujifunza na kufundishia, wakati wa hafla ya kukabidhi kompyuta hizo iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Semkiwa wilayani humo.

“Namna pekee mnayoweza kuonesha shukrani kwa wafadhili walioleta msaada shuleni kwenu ni kusoma kwa bidii na kuendelea kufanya vizuri katika masomo yenu,” amesema.

Katika hafla hiyo, shule ya Sekondari Semkiwa  ya  Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Shule ya Sekondari Kwaluguru ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni zimekabidhiwa Kompyuta 25 kila moja.

Kwa upande wa Mkoa wa Pwani wanufaika ni Shule ya Sekondari Rafsanjani Soga  iliyopo katika Halmashauri ya Mji Kibaha na Shule ya  Sekondari Simbani, iliyopo katika Halmashauri ya Kibaha ambapo kila shule itapata kompyuta 25.

Mwakilishi wa Camara Education Tanzania, Asia Bonanga amesema shirika hilo linajikita katika kupeleka teknolojia ya mawasiliano shuleni ili  kusaidia jitihada za kupatikana kwa elimu bora nchini.

Amesema  maono ya  Camara Education Tanzania ni  kuona hakuna mwanafunzi anayeachwa nyuma  katika Tehama.

Kaimu Mkurugenzi wa Miradi na Utafutaji Rasilimali  na Usimamizi wa Miradi  kutoka TEA,  Masozi Nyirenda ameshukuru shirika hilo kwa msaada huo wa kompyuta na kukumbusha shule zilizonufaika kuzitumia na kuzitunza vizuri ili zidumu na kunufaisha kundi kubwa la wanafunzi.

“Kama tunavyofahamu vifaa hivi vinahitaji utunzaji maalum ikiwa ni pamoja na kuwa na vyumba vinavyofaa, hivyo shule nufaika zijiandae vyema kwa hili,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button