Tamasha la watoto wanaoishi mazingira magumu laiva

KILIMANJARO; Zaidi ya watoto 2,000 wanaoishi katika mazingira magumu wanatarajiwa kushiriki Tamasha la Kwanza la Michezo litakalofanyika Juni 21, 2026 katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), mkoani Kilimanjaro.

Tamasha hilo limeandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la KIDEP Foundation linalojihusisha na malezi na ustawi wa yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu, kwa lengo la kuibua vipaji, kukuza ushirikiano na kuwajengea watoto hao kujiamini.

Akizungumza leo mjini Moshi wakati wa maandalizi ya tamasha hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro, Nelson Mrashani, amesema tukio hilo ni la kwanza kufanyika mkoani humo na linatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya michezo, hususan riadha.

Amesema tamasha hilo litahusisha riadha pamoja na michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, uimbaji na maonesho ya vipaji tofauti, hali itakayowapa watoto nafasi ya kuonesha uwezo wao mbele ya wazazi, walezi na wadau wa maendeleo.

“Tamasha hili linawakutanisha waliopo kwenye vituo vya kulelea watoto pamoja na wale wanaoishi majumbani ili wapate nafasi ya kujuana, kubadilishana uzoefu na kujiona kuwa wao pia ni sehemu ya jamii. Tunataka wajione hawana tofauti yoyote na watoto wengine,” amesema Mrashani.

Ameongeza kuwa baadhi ya watoto wanaotarajiwa kushiriki waliwahi kushiriki mashindano ya UMISSETA na kufanya vizuri, jambo linaloonesha kuwa wana vipaji vikubwa vinavyohitaji kuendelezwa.

Kwa mujibu wa Mrashani, wageni mbalimbali wanatarajiwa kushiriki tamasha hilo akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mkuu wa Wilaya, wazazi, walezi, pamoja na wadau wengine wa maendeleo ya watoto.

Kwa upande wake, ofisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Moshi, Duncan Mgati, ametoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki tamasha hilo ili kuwapa watoto hao hamasa na kuwafanya wajione kuwa wanathaminiwa na jamii.

Amesema mbio hizo zitafanyika katika umbali wa kilomita 10, kilomita 5 na kilomita 2, huku akieleza kuwa tamasha hilo linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji na kuimarisha mshikamano miongoni mwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button