Watu 500 kushiriki wiki ya Azaki
TAKRIBANI washiriki 500 kutoka maeneo tofauti nchini na nchi jirani, wanatarajia kushiriki wiki ya Asasi Za Kiraia (AZAKI), mkoani Arusha itakayofanyika Oktoba 24 hadi 28, mwaka huu.
Akizungumza mkoani Dar es Salaam Alhamis, mratibu wa wiki ya Azaki 2022, Dk Shirley Mushi alisema usajili wa ushiriki mwaka huu ni kwa njia ya mtandao na kwamba kushiriki tukio hilo la wiki moja, washiriki wajiandikishe mapema ili kupata nafasi.
“Wiki ya Azaki 2022 itawapa kipaumbele wananchi kwenye kila shughuli na mijadala itakayofanyika. Wiki ya Azaki mwaka huu, itaonesha mbinu fanisi na ubunifu wa sekta hii kama mdau muhimu wa maendeleo,” alisema.
Alisema Kamati Tendaji ya Wiki ya Azaki 2022 na waandaaji walizindua rasmi shughuli hiyo yenye kaulimbiu ‘Maendeleo ya Watu, Simulizi za Watu’ inayosisitiza kwamba, watu ndio sehemu kuu ya malengo ya Azaki na uwapo wake.
“Kaulimbiu hii inaruhusu kutafakari kwa kina juu ya mbinu, mifumo na michakato mingi inayotumiwa na Azaki kutatua changamoto ambazo Watanzania wanakabiliana nazo,” alisema.
Dk Mushi alisema ajenda ya mwaka huu ya wiki ya Azaki itaelekezwa katika kuhakikisha watendaji wa sekta mbalimbali wanaimarisha ushirikiano na mahusiano yanayolenga kuleta maendeleo.



