Wananchi kupimwa bure magonjwa ya moyo

DAR ES SALAAM; HOSPITALI ya DSB Polyclinic kwa kushirikiana na Taasis ya Heart of Foundation of Tanzania, zimeandaa kambi ya siku mbili ya utoaji wa huduma ya upimaji na matibabu bila malipo ya magonjwa ya moyo na magonjwa mengine kwa watu wazima na watoto Dar es Salaam.
Kambi hiyo inaanza kesho Novemba 4, 2023 kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 11 jioni katika hospitali ya DSB Upanga na watakaokutwa na matatizo watapatiwa dawa.
Daktari kiongozi wa DSB, Issa Mbashu amesema huduma zitakazotolewa katika kambi hiyo ni pamoja na upimaji wa shinikizo la damu, upimaji wa sukari kwenye damu, upimaji wa uwiano wa urefu na uzito, upimaji wa oksijeni mwilini na kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo.
Amesema vipimo vingine ni kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, kipimo cha msongo wa mawazo (stress), ushauri wa daktari bingwa wa moyo, elimu na ushauri wa lishe bora na upatikanaji wa dawa kwa wale watakaokutwa na matatizo kupatiwa dawa.
Amesema kambi hiyo inafuatia maadhimisho ya siku ya kiharusi duniani yaliyofanyika Oktoba 29, na kuwataka wananchi kufika kwa wingi ili kupata matibabu.



