Washiriki mafunzo NBAA watakiwa kuboresha ufanisi

DAR ES SALAAM: Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), imehitimisha mafunzo ya siku mbili yaliyokuwa yakiendelea kwa wataalamu wa uhasibu kutoka taasisi mbalimbali, ikiwa na lengo la kuboresha utungaji na usahihishaji wa mitihani kwa kuzingatia viwango vipya vya mitaala, ili kuimarisha ubora wa wahasibu nchini.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo Septemba 12, 2024, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Pius Maneno amewapongeza washiriki kwa kujitolea kujifunza mbinu mpya na teknolojia zinazohusiana na utungaji wa mitihani.

Amesisitiza kuwa umuhimu wa wataalamu wa uhasibu kutumia maarifa waliyoyapata kusaidia wengine na kuboresha sekta nzima ya uhasibu nchini, ili kuleta tija katika soko la ajira duniani na kuchagiza katika ukuaji wa uchumi.

Soma pia: Wahasibu watakiwa kuzingatia maadili

“Mmepewa nyenzo muhimu ambazo zitawasaidia kufanya maamuzi bora katika utungaji wa mitihani na usimamizi wa ubora, tunahitaji ujuzi wa msingi na sio maarifa tu, ili kuwapata wahitimu wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko la ajira, hii inamaanisha tunajaribu zaidi vipaji na ujuzi kuliko maarifa ya nadharia pekee,” amesema CPA Maneno.

Amewataka wataalamu hao kuwa mabalozi wa mabadiliko katika mitihani ya uhasibu, hivyo mitihani inapaswa kupima ujuzi halisi na sio kutumia teknolojia kama akili mnemba(AI) inayoweza kutoa majibu ya nadharia, ambayo hayapimi uwezo wa mwanafunzi

Habari Zifananazo

Back to top button