Wahandisi washauriwa kuungana kuongeza tija

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewashauri wahandisi kuungana na kuomba zabuni kwa umoja ili kuongeza tija na ushindani kwenye mnyororo wa sekta hiyo.
Akizungumza katika mkutano wa tano wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu na Wakadiriaji Majengo (Architects and Quantity Surveyors Registration Board), Jijini Dar es Salaam, Mpogolo amesema ni muhimu kwa wataalamu wa ndani kutumia uwezo wao katika miradi ya serikali ili kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje.
Amebainisha kuwa, ingawa wataalamu wa ndani wanakabiliwa na changamoto ya mitaji midogo, wanapaswa kuongeza juhudi zao kushiriki katika miradi hiyo badala ya kuruhusu serikali kutumia wataalamu wa nje, hali inayosababisha upotevu wa fedha za kigeni.
Amehimiza wataalamu wa ndani kushirikiana kwa kuondoa ubaguzi katika utoaji wa fursa za kazi ili kufanikisha miradi hiyo kwa umoja.
Aidha, Mpogolo amekemea tabia ya baadhi ya wataalamu wa ndani kuwatafuta wataalamu wa nje na kushirikiana nao huku wao wakipata sehemu ndogo ya faida. Alisisitiza kuwa mshikamano na ushirikiano wa kitaifa ni muhimu katika kufanikisha maendeleo ya sekta ya ujenzi na kuimarisha uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa wabunifu na Wakadiriaji wa Majengo (Architects and Quantity Surveyors Registration Board) Dk Ludigija Bulamile amesema kuna ongezeko la wabunifu majengo wenye ustadi na ubunifu mkubwa katika kuleta matokeo chanya, lakini pia wamekuwa na juhudi katika kuwatafuta wahitimu na kuwapatia mafunzo na wamefanikiwa kuwapatia elimu watihimu katika sekta hiyo.
Kongamano hilo lililenga kujadili changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya ujenzi, pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye miradi mikubwa inayotekelezwa na serikali.



