Takukuru Manyara waokoa mil 13/-

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara imeokoa zaidi ya Sh milioni 13 ambapo milioni 4.8 zilitokana na thamani ya dawa zilizokuwa zimeibiwa kwenye Zahanati ya Orkirung’rung na kurejeshwa baada ya kufanyika ufuatiliaji wa taasisi hiyo.
Taarifa hiyo imetolewa leo Novemba 19, 2024 na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Manyara, Bahati Haule wakati akitoa taarifa ya tathmini ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kuanzia Julai hadi September mwaka mwaka huu.
Aidha mpango wa Takukuru Mkoa wa Manyara kwa mwaka 2022/23 hadi 2025/26 utaimarisha juhudi za kuzuia rushwa kwa kufuatilia na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kuzuia rushwa kupitia uelimishaji ikiwemo klabu za wapinga rushwa shuleni.
Amesema kuelekea uchaguzi wa viongozi wa Serikali zà Mitaa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya atakayebainika kutoa na kupokea rushwa..
Amesema kwa mujibu wa ibara ya (4) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na kwamba ibara ya (9)inasema Moja kati ya jukumu kubwa la Serikali ni kuondoa Rushwa nchini huku ibara ya (8)inasema serikali itapata madaraka kutoka kwa wananchi na itawajibika kwa wananchi.
Kwa mujibu wake lengo kuu ya ibara hiyo ni kuimarisha demokrasia na wananchi wajue kwamba wanatakiwa kutumia demokrasia kuharikisha maendeleo ya taifa.
“Tunakemea rushwa kwenye uchaguzi rushwa ni kosa la jinai, ni kosa la kiimani,maandiko matakatifu kwenye vitabu vyote vya dini vinakataza pia ni kosa kwa mujibu wa utumishi wa umma,” amesisitiza Haule.



