Vodacom, Sanlam zaja na mpango wa kuwekeza kidijitali

DAR ES ES SALAAM: Kampuni ya mawasiliano, Vodacom Tanzania Plc imeungana  kwa kushirikiana na Sanlam Investments East Africa Limited, leo wamezindua M-Wekeza, huduma ya kibunifu ya uwekezaji iliyoundwa ili kuleta fursa rahisi za uwekezaji kwa watumiaji wa M-Pesa kupitia njia ya kidijitali ya simu zao za mkononi.

M-Wekeza inawawezesha watumiaji kuanza kuwekeza kwa kiasi cha 10,000/-, ikitoa faida ya ushindani ya hadi asilimia 13 ya riba kwa mwaka. Huduma hii ya kisasa inaashiria kuingia kwa Vodacom M-Pesa katika masoko ya mitaji, ikileta fursa mpya za ukuaji wa kifedha kwa Watanzania na kuendeleza dhamira ya kampuni hiyo ambayo ni kukuza ushirikishwaji wa kifedha.

Huduma hii inayoletwa kwa kushirikiana na Sanlam Investments East Africa Ltd, mshirika wa uwekezaji aliye na leseni na sifa nzuri, inalenga kurahisisha mchakato wa uwekezaji kwa kila Mtanzania, na kuwawezesha kuongeza kipato chao kwa kuwekeza kwenye vyombo kama dhamana za serikali, masoko ya hisa na masoko mengine ya mitaji salama.

Huduma hii inaendana na malengo ya Vodacom ya kukuza ushirikishwaji wa kifedha na kutoa huduma mbalimbali za kifedha kupitia M-Pesa.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Mkurugenzi wa M-Pesa Epimack Mbeteni alielezea kuzinduliwa kwa huduma hiyo ni hatua nyingine muhimu katika
dhamira yetu ya kuwawezesha Watanzania, kwa kutoa huduma mbalimbali za kifedha kidigitali.

“Tumebuni huduma hii ili iwe rahisi, ipatikane kwa wote na yenye kuwaletea faida. Iwe wewe ni mwekezaji mzoefu au mpya, M-Wekeza inatoa fursa salama na rahisi ya kuongeza kipato chako kupitia simu yako ya mkononi, amesema.

SOMA: Vodacom Tanzania yazindua huduma za 5G

M-Wekeza inadhibitiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Usalama (CMSA), ambayo inahakikisha uwazi na usalama hivyo kuleta imani kubwa katika mchakato wa uwekezaji.

Kwa usimamizi imara kutoka CMSA, M-Wekeza inatoa njia salama na ya kuaminika kwa watumiaji wa M-Pesa kushiriki katika masoko ya mitaji yanayokua ya Tanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa CMSA, Nicodemus Mkama, alisisitiza umuhimu wa huduma  kwa kusema kuwa; “Uzinduzi wa M-Wekeza ni hatua ya mabadiliko kuelekea kurahisisha upatikanaji wa fursa za uwekezaji hapa Tanzania. Ushirikiano huu kati ya Vodacom, Sanlam Investments na CMSA unaleta daraja linalowaunganisha Watanzania na masoko ya mitaji na hivyo kuwawezesha watu kutoka tabaka zote za kijamii kuwekeza na kujenga mustakabali wao wa kifedha.”
Jonathan Stichbury, Mkurugenzi Mtendaji wa Sanlam Investments East Africa alisema: “Sanlam Investments, tumejidhatiti kukuza ushirikishwaji wa kifedha.”

 

Habari Zifananazo

Back to top button