Namibia kutegemea kupata Rais mwanamke

NAMIBIA : NCHINI Namibia wananchi wanajiandaa kupata rais wa kwanza mwanamke huku theluthi mbili ya kura za uchaguzi zikiendelea kuhesabiwa na kumuweka mgombea wa chama tawala cha SWAPO kifua mbele kushinda uchaguzi huo.
Makamu wa rais Netumbo Nandi-Ndaitwah kutoka chama tawala ambacho kimeshika madaraka miaka 34 iliyopita, amepata zaidi ya asilimia 54 ya kura, kulingana na hesabu ya tume ya uchaguzi ni karibu asilimia 66 ya kura zilizopigwa.
Kiongozi wa upinzani Panduleni Itula wa chama cha Independent Patriots for change (IPC), ameachwa mbali na asilimia 28 ya kura.
Itula, mwenye umri wa miaka 67, amesema kulikuwa na mapungufu mengi katika uendeshaji wa uchaguzi.
“mapungufu yamekuwa ni mengi IPC haitakubali matokeo ya uchaguzi huu.”
Alisema, “Sheria ya utawala imeshindwa kabisa na hatuwezi kuita uchaguzi huu kuwa huru, haki, na wa halali kwa vyovyote vile.”
Uchaguzi wa tarehe 27 Novemba ulilazimika kuahirishwa mara mbili kutokana na matatizo ya kiufundi na ya usafiri, ikiwa ni pamoja na upungufu wa karatasi za kupigia kura, hali iliyosababisha foleni ndefu ambapo baadhi ya wapiga kura walilazimika kukata tamaa baada ya kusubiri kwa saa 12.
Nandi-Ndaitwah, mwenye umri wa miaka 72, anaweza kulazimika kwenda kwenye duru ya pili ya uchaguzi ikiwa hatapata zaidi ya asilimia 50 ya kura wakati matokeo yote yatakapotangazwa.
Ikiwa atashinda, atakuwa rais wa kwanza mwanamke wa nchi hii yenye watu takribani milioni tatu, inayojulikana kwa ukame na mazingira ya hali ya hewa ya jangwa.
Matokeo yaliyotangazwa mapema Jumanne yalikuwa ya majimbo 79 kati ya 121, ikiwa ni pamoja na karibu majimbo yote ya mji mkuu Windhoek. SOMA: Miss Namibia autaka urais
Kwa jumla, wapiga kura milioni 1.5 walisajiliwa, 73 walipiga kura, kwa mujibu wa tume ya uchaguzi.
Netumbo Nandi-Ndaitwah akitangazwa mshindi rasmi wa urais atakuwa rais wa tatu mwanamke barani Afrika.



