Jukwaa laendelea kuelimisha wanawake ukatili kijinsia

JUKWAA la Wanawake Mkoa wa Mtwara (JUWAM) limeendelea kutoa elimu kwa wanawake zaidi ya 200 kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia pamoja na makuzi ya mtoto katika kijiji cha kawawa kata ya Mkunwa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara.
Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo hasa makuzi ya mtoto mwenyekiti wa jukwaa hiyo hilo, Mariamu Chimbwahi amesema makuzi ya mtoto yanaanzia tangu mtoto akiwa tumboni kwa mama kabla hajazaliwa.
Elimu hiyo imetolewa leo Disemba 6, 2024 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, elimu iliyotolewa katika kijiji hicho cha kawawa kata ya Mkunwa kwenye halmashauri hiyo.

Hata hivyo makuzi yanategemea namna ambayo wazazi wanawalea watoto hivyo wamesisitizwa kuweka jitihada kwenye malezi bora ya mtoto ili aweze kukua katika misingi ya kimaadili kinyume na hapo anakuwa akiwa na tabia isiyokuwa njema na baadhi yao kujiingiza katika vitendo vihofu kama vile matumizi ya madawa ya kulevya.
‘’Na suala la malezi siyo tu jukumu la mama pekee bali hata akina baba kwahiyo tujitahidi kushirikiana na wazazi wenzetu kuwalea watoto wetu katika makuzi mazuri kwakuwa hakuna mzazi ambaye anataka mtoto wake akizaliwa awe na tabia mbaya, kila mzazi anataka mtoto wake awe na tabia mzuri kuanzia nyumbani hadi shuleni’’amesema Chimbwahi.

Katibu wa jukwaa, Judith Chitanda amezungumzia suala la vitendo vya ukatili vinavyofanywa na baadhi ya watu katika jamii yao hivyo amewaomba wanawake hao kuwa, kutofumbia macho pale wanapoona vitendo hivyo vikifanyika kwenye jamii.
‘’Akina mama ninyi wenyewe mnajua watoto wetu wanabakwa na kulawitiwa, kikubwa tumeona tuje kwenu kwasababu akina mama ndiyo walezi kwahiyo lazima tuzingatie malezi ya watoto tunapoona vitendo hivi lazima tuviripoti, vikiripotiwa wengine wanaotamani kuvifanya hawawezi wataongopa’’amesema Chitanda
Mmoja wa wanawake hao akiwemo Betina Endrick mkazi wa kijijini hapo, amelipongeza jukwaa hilo kwa kuwaletea elimu hiyo ya malezi bora kwa watoto ambayo itaenda kuwasaidia katika kuwalea watoto wao lakini pia wataripoti vitendo vya ukatili vitapojitokeza kwenye jamii yao.

Aidha jukwaa hilo linatekeleza majukumu yake hayo kipitia mradi wa ‘Sauti Zetu’ kwenye kata tatu zilizopo wilayani humo ikiwemo Vigaeni, Naumbu na Msangamkuu kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la Women Fund Tanzania Trust (WFT) lililopo Jijini Dar es Salaam.
Mradi huo ulianza kutekelezwa Julai 2024 na unamaliza Disemba mwaka huu ambapo moja ya majukumu yake ikiwemo kutoa elimu ya mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono.
Hata hivyo mpaka sasa tangu kuanza kwa mradi huo jumla ya midahalo mitatu imefanyika na kufanikiwa kuwafikia wanawake zaidi ya 800 kwenye maeneo hayo yanayotekelezwa mradi.


