Simba, Singida patamu leo

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba leo watakuwa wageni wa Singida Black Stars kwenye mchezo wa ligi hiyo Uwanja wa Liti mkoani Singida.
Simba wanaongoza ligi hiyo baada ya kukusanya pointi 37 kwenye michezo 14 iliyocheza, wakifunga mabao 30 na kuruhusu wavu wao kuguswa mara tano.
Ndio timu yenye safu bora ya ulinzi na ushambuliaji kwa mujibu wa takwimu kwenye Ligi Kuu mpaka sasa huku Singida wenyewe wanashika nafasi ya nne wakiwa na pointi 33, wakifunga mabao 22 na kuruhusu mabao 10 kwenye mechi 15 walizocheza mpaka sasa.
Kama Simba wataibuka na ushindi kwenye mechi ya leo watafikisha pointi 40 na kuwaacha wapinzani wao Yanga wanaoshika nafasi ya pili na ambao kesho wanacheza na Fountain Gate kwa tofauti ya pointi nne lakini Wekundu hao wa Msimbazi wakiwa mbele kwa mchezo mmoja.
Ushindi kwa Singida Black Stars utawafanya kufikisha pointi 36 na kuishusha Azam kwenye nafasi ya tatu kwa tofauti ya pointi tatu lakini wakiwa wamecheza mchezo mmoja zaidi.

Akizungumza kuelekea mchezo huo Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids alisema wamejiandaa vizuri na malengo yao kukusanya pointi tatu zitakazowafanya kuendelee kukaa kileleni.
“Tuko kwenye hatua ambayo tukiteleza kidogo tu wapinzani wetu wanaweza kuongoza ligi kama watashinda mchezo wao, hivyo huu ni mchezo muhimu kwetu kushinda kama ilivyo michezo mingine na wachezaji wangu wanajua umuhimu wa huu mchezo,” alisema Fadlu.
Kwa upande wake Kocha wa Singida Black Stars, Ramadhani Nsanzurwimo alisema wamejipanga kuutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani kupata pointi tatu dhidi ya Simba.
“Tuko nyumbani na mtu ukiwa nyumbani kwako unaweza kutumia silaha yoyote kupata ushindi. Simba ni timu kubwa, hivyo tunajua kama tunaweza kudhibiti kucheza kwa presha tunaweza kupata ushindi, hatutaki presha kwenye timu yetu na hicho ndicho kitu tumetengeneza kwenye timu yetu,” alisema Nsanzurwimo.



