Huyu ndiye Stephen Wasira

SHANGWE na nderemo ziliibuka wakati Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan akimtangaza kada mkongwe wa chama hicho, kuwa Makamu Mwenyekiti CCM Tanzania Bara, Stephen Wa sira (80) na baadaye kupitishwa na wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa chama hicho kwa kupata asilimia 99.42 ya kura zilizopigwa.
NEC ilifikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha juu ya tabia, mwenendo na sifa za mwanachama huyo kwa muda wote wa uhai wake ndani ya CCM.
Wasira ni nani
Wasira alizaliwa 1945 wilayani Bunda Mkoa wa Mara na kuanza safari ya ma somo katika Shule ya Msingi Bariri kuanzia 1956 hadi 1959.
Alihamia katika Shule ya Msingi Nyambitilwa kuanzia 1960 hadi 1961 na kuhitimisha elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Kisangwa 1962 – 1963. Kati ya 1964 na 1967, alihitimu elimu ya sekondari.
Alisomea Chuo cha Ukufunzi Uingereza. Kwa upande wa maisha ya utumishi, Wasira alifanya kazi akiwa msaidizi wa masuala ya maendeleo ya jamii na alianza kukitumikia Chama cha Tanu akiwa Katibu wa wilaya mwaka 1967 hadi 1973 na 1975 hadi 1982 alihudumu nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Baadaye, 1982 aliteuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Ubalozi wa Tanzania Washington DC na aliporejea nchini aliteuliwa na Rais wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani mwaka 1990 hadi 1991.
Kati ya 1993 na 1995 alisoma Shahada ya Uzamili ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Marekani.
Akiwa na umri wa miaka 25, Wasira alianza kutumikia wadhifa wa ubunge, hii ilikuwa mwaka 1970 aliposhinda ubunge wa Mwibara na kuwakilisha bungeni jimbo hilo hadi 1975. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alimteua kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
1985 aligombea na kushinda ubunge wa Bunda na kisha kuteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa na baadaye Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo mwaka 1989 hadi 1990.
Hata hivyo, 1995 aliangushwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM na Jaji Joseph Warioba ndipo aliamua kwenda NCCR Mageuzi na akachaguliwa kwa kura 18,815 dhidi ya 17,527 za Warioba.
Warioba alikata rufaa Mahakama Kuu ambayo ilitengua ushindi wa ubunge wa Wasira 1996 baada ya kujiridhisha kuwa kulikuwa na rafu nyingi zilizofanyika.
Uchaguzi mdogo ulipo fanyika mwaka 1999 Wasira hakushiriki na baadaye aliamua kurejea CCM na 2005 alirejea katika ulingo wa siasa na kisha kupita bila kupingwa katika jimbo la Bunda.
Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Maji Januari 2006 hadi Oktoba 2006 na baadaye Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika hadi mwaka 2010. Alikuwa miongoni mwa watia nia wa urais kupitia CCM mwaka 2015.