Wizara yawekeza mapambano magonjwa ya moyo

WIZARA ya Afya imewekeza zaidi katika sekta ya afya ili kupambana na magonjwa ya moyo, ambayo Shirika la Afya Duniani (WHO) linaonesha kusababisha vifo vya watu milioni 17.9 kila mwaka, sawa na asilimia 32 ya vifo vyote duniani.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa Kliniki ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Waziri wa Afya Jenista Mhagama amesema magonjwa ya moyo, hasa mshtuko wa moyo na kiharusi, yanasababisha asilimia 85 ya vifo hivyo.

Ameeleza kuwa, Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza vifaa tiba vya kisasa kama MRI, CT-Scan, na Ultrasound, pamoja na mashine za upasuaji wa tundu dogo (Cathlab carto), ambazo zimepunguza muda wa wagonjwa kukaa hospitalini.

Aidha, Waziri Mhagama amesisitiza kuhusu upanuzi wa huduma za matibabu ya moyo katika hospitali za kanda kama Chato, Benjamini Mkapa, na Mtwara, hatua inayolenga pia kukuza utalii wa tiba nchini.

Pia ameeleza kuwa programu ya tiba mkoba ya Dk Samia Suluhu Hassan imeimarisha huduma za kibingwa katika maeneo mbalimbali.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mkakati wa bima ya afya kwa wote unaendelea, na amewataka wananchi kuungana katika kuhamasisha umuhimu wa bima hiyo kama njia ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa JKCI Dk Kisenge amesema taasisi hiyo ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 300 wa upasuaji wa tundu dogo na 800 wa upasuaji wa kifua kwa siku, huku wakiweka malengo ya kuhudumia wagonjwa 3,500 wa upasuaji wa tundu dogo na 900 wa upasuaji wa kifua kila mwaka.

Habari Zifananazo

Back to top button