Wapalestina wagoma kuhamishwa GAZA

PALESTINA : KIONGOZI wa Palestina Mahmud Abbas na kundi la Hamas wamekataa kukubaliana na mapendekezo ya kuwaondoa wakaazi wa Gaza kutoka eneo hilo lililokumbwa na vita baada ya wazo la Rais wa Marekani Trump la kusafisha eneo hilo.

Baada ya miezi 15 ya vita, Trump amesema Gaza imekuwa eneo la ubomoaji kwahiyo kunahaja ya kuwahamisha  Wapalestina nje ya  eneo hilo.

Ofisi ya Rais Abbas iliyoko Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, imepinga na kulaani mipango yoyote inayolenga kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza.

Taarifa inasema kuwa Wapalestina hawataitelekeza ardhi yao na maeneo matakatifu. SOMA: ISRAEL: Baraza kupiga kura kusitisha mapigano Gaza

Bassem Naim, mwanachama wa ofisi ya kisiasa ya Hamas amesema Wapalestina watazuia miradi ya aina hiyo kama tu walivyofanya katika miongo mingi iliyopita.

Kundi la Islamic Jihad linalopigana pamoja na Hamas huko Gaza limesema wazo la Trump ni la kusikitisha na linahimiza uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Pendekezo hilo pia limepingwa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Ayman Safadi amesema uamuzi wao wa kupinga uhamishwaji wa Wapalestina ni thabiti na hautabadilika.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ilisema inakataa ukiukwaji wowote wa haki zisizoweza kuguswa za Wapalestina, ikiwa ni pamoja na kukaa au kunyakua ardhi, au kwa kuondolewa kwa ardhi ya watu wake kwa njia ya uhamisho, au kuhimiza uhamisho au kung’olewa kwa Wapalestina kutoka ardhi yao, iwe kwa muda mfupi au kwa muda mrefu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button