Dk Mpango akutana na Naibu Mkurugenzi Mtendaji IMF

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bo Li.
Mazungumzo hayo yamefanyika kando ya Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika unaofanyika leo Januari 28 jijini Dar es Salaam.

Katika Mazungumzo hayo, Makamu wa Rais ameishukuru IMF kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania kupitia programu mbalimbali ikiwemo dirisha la mikopo nafuu ya nyongeza ya kuchochea kasi ya kuimarisha uchumi baada ya Janga la UVIKO-19 na changamoto zitokanazo na vita (Extended Credit Facility – ECF) pamoja na programu ya kuimarisha uwezo wa nchi kukabiliana changamoto zitokanazo na athari za mabadiliko ya tabianchi (Resilience and Sustainability Facility-RSF).
Amesema programu hizo zimechangia ukuaji wa uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei na ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa IMF Bo Li ameipongeza Tanzania kwa kuimarisha uchumi na kufanikisha utekelezaji wa programu za ushirikiano ikiwamo programu kupitia ECF na RSF.
Aidha ameipongeza Tanzania kwa kutekeleza vyema programu ya ECF na kupata alama za juu katika tathimini ya nne.

Aidha, Li ameipongeza Tanzania kwa kuwa nchi ya mfano iliyochaguliwa pamoja na Madagascar kutekeleza mpango kabambe wa utafutaji wa fedha za mazingira kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwamo sekta binafsi, washirika wa maendeleo na AZAKI.



