Trump afungiwa kusitisha ufadhili wa serikali

MAREKANI : JARIBIO la Rais wa Marekani, Donald Trump, kufungia mamia ya mabilioni ya dola katika ufadhili wa serikali limezuiliwa kwa muda na mahakama.
Mpango wa Trump ulisababisha mparaganyiko mkubwa serikalini na kuzua hofu kwamba utaathiri vibaya programu muhimu zinazowahudumia mamilioni ya Wamarekani.
Dakika chache kabla ya utekelezaji wa mpango huo jana jioni, jaji wa shirikisho alitoa agizo la kusitisha mpango huo wa Trump, ambao ungeathiri maelfu ya programu za ruzuku za serikali na mikopo kwa wananchi.
Uamuzi wa Trump wa kusitisha misaada mbalimbali unatajwa kuwa utatatiza maendeleo katika sekta za elimu, huduma za afya, makaazi, misaada ya majanga, na programu nyingine muhimu za kijamii.
Agizo hilo ni utekelezaji wa ahadi za Trump alizozitoa katika kipindi cha uchaguzi, ambazo zililenga kufanya mabadiliko makubwa katika utawala wa serikali kuu.
Hadi sasa, Rais Trump tayari amezuia misaada mingine ya kigeni na kusimamisha ajira za wafanyakazi wa serikali. SOMA: Biden hana imani na serikali ya Trump
Wademocrat wamekosoa vikali hatua hiyo, wakisema inashambulia mamlaka ya Bunge juu ya matumizi ya serikali, huku wakionyesha wasiwasi kuhusu kuchelewa kwa malipo kwa madaktari na walimu wa shule za chekechea.
Hata hivyo, Warepublican wameitetea hatua hiyo, wakisema inatekeleza ahadi ya Trump ya kudhibiti bajeti ya Marekani inayokaribia $6.75 trilioni.



