Rais Tshisekedi hatohudhuria mkutano wa EAC

CONGO : NAIBU Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano cha Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Giscard Kusema, amesema Rais Félix Tshisekedi hatahudhuria mkutano wa dharura ulioitishwa na Rais William Ruto wa Kenya, kuzungumzia mgogoro unaoendelea mashariki mwa Congo.
Kusema alisema kuwa Tshisekedi anafuatilia kwa karibu matukio ya mashariki mwa Congo, lakini hana mipango ya kuhudhuria mkutano huo badala yake Rais Tshisekedi atatoa hotuba jioni kupitia matangazo ya moja kwa moja kutoka ofisi zake.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais William Ruto, aliiitisha mkutano wa dharura tarehe 29 Januari ili kujadili mzozo unaoendelea mjini Goma, mashariki mwa DRC. Ruto alisema alizungumza na Rais Tshisekedi na Rais Paul Kagame wa Rwanda, ili kutafuta suluhu kwa hali hiyo.
Rwanda imekuwa ikilaumiwa kwa kuhusika na mzozo unaozidi kushika kasi mjini Goma, kutokana na madai ya kuunga mkono waasi wa vuguvugu la Machi 23.
SOMA: EAC kujadili mgogoro wa DR Congo



