Dira 2050 yaitaka Tanzania imara EAC, SADC, AU

RASIMU ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeeleza kuwa ni muhimu Tanzania iimarishe uongozi wake ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (UA).

Imeeleza kuwa hilo linawezekana kwa kuandaa sera za kikanda kwa kuimarisha biashara na uwekezaji. Rasimu hiyo imeeleza kuwa hilo likifanyika, itaimarisha diplomasia ya utamaduni wa Tanzania na kuipa nguvu na kuifanya kuwa kivutio cha utalii, kubadilishana utamaduni na elimu.

Rasimu hiyo imeeleza kuwa utekelezaji madhubuti wa Mkakati wa Diplomasia ya Utamaduni utainua hadhi ya Tanzania na kuimarisha uhusiano wake kimataifa.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuiweka Tanzania kama daraja kati ya Afrika Mashariki na Kati na masoko yanayochipukia Asia na Amerika ya Kusini kuvutia uwekezaji, uhamishaji wa teknolojia na kupanua fursa za biashara za nje.

Rasimu hiyo pia, inaelekeza kukuza sauti ya Tanzania kuhusu masuala ya kimataifa kama biashara, maendeleo endelevu na hali ya hewa.

Matarajio ya dira hiyo ni kuongeza ushirikiano na uongozi katika ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika, kupitia mipango inayoendelea ya kujenga amani, upatanishi na kuongeza ushawishi katika mifumo ya sera za usalama wa kikanda.

Pia, Dira ya 2025 inatarajia ushirikiano thabiti wa kimkakati uliojengwa kwenye misingi ya uhusiano wa kiuchumi na kidiplomasia na nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi, kwa lengo la kuwezesha uwekezaji na uhamishaji wa teknolojia.

Dira hiyo inalenga uimarishaji wa masuala ya kiutamaduni, ikiwa ni pamoja na kukuza Kiswahili kama lugha ya kikanda na kimataifa na uzoefu wa kitamaduni na kuwa kiungo muhimu kimataifa katika kutetea maslahi ya Afrika katika majukwaa ya kimataifa kuhusu masuala muhimu kama vile haki za bindamu, mabadiliko ya tabianchi, haki ya kiuchumi na maendeleo endelevu.

Dira inasema, kuwa na sekta binafsi yenye nguvu na inayowajibika ni injini ya uchumi imara na endelevu. Inaeleza kuwa jitihada zimefanywa kushirikisha na kukuza ushiriki wa sekta binafsi, ikiwa ni pamoja na majadiliano ya sekta ya umma na binafsi na kuanzishwa kwa mfumo na sera ya ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi.

Pia, diplomasia ya kiuchumi imekuwa ni kipengele muhimu katika sera ya mambo ya nje pamoja na mipango kadhaa
ya ujumuishaji wa kifedha imetekelezwa ili kuongeza upatikanaji wa mtaji wa kifedha.

Dira inabainisha kuwa kumekuwa na jitihada za kuandaa sera ya taifa inayohimiza matumizi ya rasilimali za ndani katika miradi ya maendeleo kama njia mbadala ya ushiriki mdogo wa kampuni za ndani katika miradi ya uchumi kwa sababu mafanikio ya sera hiyo yatategemea ufanisi katika utekelezaji na usimamizi.

Matarajio ya Dira ya 2050 katika sekta binafsi imara ni kuwa na huduma ya umma inayolenga sekta binafsi ili kukuza mazingira wezeshi ambapo biashara binafsi zinaweza kustawi na kuchangia kwa ufanisi katika maendeleo ya kiuchumi.

Pia, inatarajia kuwa na sekta binafsi yenye ushindani, imara na jumuishi ambayo inaongoza maendeleo ya kijamii na
kiuchumi na sekta inayoweza kushindana katika soko la kimataifa kwa kutumia nafasi iliyonayo katika mnyororo wa
thamani kimataifa.

Aidha, matarajio mengine ni kupungua kwa kiasi kikubwa idadi ya sekta zisizo rasmi katika uchumi. Mashirika ya umma Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaeleza kuwa mashirika ya umma yana mchango mkubwa kwenye uchumi hususani kwa sekta zenye masilahi makubwa ya taifa.

Inaeleza kuwa mashirika mengi kwa sasa hayaendeshwi kwa ufanisi na faida, hali inayochangiwa na kukosekana kwa uhuru wa uendeshaji na fedha na hivyo kuendelea kuwa mkondo wa kutumia fedha za umma.

Pia, rasimu hiyo inaeleza kuwa mashirika ya umma yanapaswa kuelekeza uwekezaji wake kwenye maeneo ya kimkakati yenye masilahi ya nchi kama vile nishati, usafirishaji na huduma muhimu za umma kwani hiyo itachangia kuweka msingi wa maendeleo mapana ya uchumi, kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi na kuongeza ufanisi wa soko.

Inasema ili kuyafanya haya, uendeshaji wa mashirika ya umma unapaswa kufanyika kwa uwazi na ufanisi, kuhakikisha ushirikiano badala ya ushindani utakaozibana sekta binafsi.

Dira ya 2050 inatarajia kuwa na mashirika ya umma ya kimkakati na yenye ufanisi na kuwa na mashirika ya umma imara yaliyojengwa kwenye msingi wa uadilifu, uwazi, uwajibikaji na usimamizi thabiti kwa lengo la kuongeza mchango wa kijamii na kiuchumi huku yakishirikiana na sekta binafsi katika kukuza uchumi jumuishi na maendeleo ya taifa.

Pia, rasimu hiyo inatarajia kuwa na mashirika ya umma yanayojiendesha yenyewe kwa faida na kuvutia uwekezaji
mpana ili kuongeza kasi ya maendeleo ya uchumi na hivyo kuwezesha utoaji wa huduma kwa umma. Inatarajia kuwa na mashirika ya umma yenye uwezo wa kushindana kitaifa na kimataifa katika soko kwa ubunifu pasipo kuathiri matumizi ya rasilimali za umma katika vipaumbele vya maendeleo.

Dira hiyo pia, inatarajia kuwa na mashirika ya umma yanayoweza kumudu ushindani wa kimataifa na kuwezeshwa
kimkakati kukuza viwanda, maendeleo ya miundombinu na ukuaji wa kiuchumi huku yakizingatia ushirikiano na sekta binafsi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button