Polisi yaanika kiini wizi wa ng’ombe Geita

JESHI la Polisi mkoani Geita limeweka wazi kuwa moja ya kiini kikubwa cha ongezeko la matukio ya wizi wa mifugo mkoani humo ni uwepo wa mabucha bubu pamoja na biashara ya nyama na chakula isiyozingatia sheria.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi (SACP) Safia Jongo ametoa taarifa hiyo kwa  waandishi wa habari na kuongeza kuwa pia wafanyabiashara wa chakula wanahusika.

Taarifa hiyo inakuja ikiwa ni siku chache tangu madiwani wa Manispaa ya Geita walipowasilisha malalamiko yao kuhusu tatizo hilo katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/25.

Kamanda Jongo ametaja wahusuka wakubwa wa matukio ya wizi wa mifugo waliobainika kuwa ni wahalifu ambao waliwahi kufungwa lakini wakamaliza kifungo chao na kurejea kufanya uhalrifu tena.

“Sisi kama jeshi la polisi tunaendelea kuwasisitiza wananchi, kujenga mazizi salama, kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi kwa maana ya sungu sungu ili tushirikiane kupambana na hao watuhumiwa.

“Lakini oparesheni mbambali zimepangwa ikiwemo kukagua mabucha kwa sababu mabucha bubu haya nayo yanachangia kuuza hizo nyama,” amesema Jongo.

Kamanda Jongo amewahakikishia wakazi wa Geita kuwa jeshi la polisi limeweka mipango thabiti kufuatilia kwa kina ili kudhibiti na kukomesha wizi wa mifugo na aina zote za uhalifu.

Akizungumza katika Kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Geita, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Barnabas Mapande ameomba hatua za haraka zichukuliwe kudhibiti wimbi hilo.

Mapande amesema kwa siku za hivi karibuni wananchi wengi ambao ni wafugaji wilayani humo wanaishi bila amani na wameripoti kuibiwa mifugo yao na hivo vyombo vya ulinzi na usalama vitatue tatizo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button