‘Valentine’s Day’: Siku inayoadhmishwa ‘kichwa chini miguu juu’

LEO ni Februari 14, 2025; Siku ya Wapendanao, wengi huiita kwa Kiingereza, ‘Valentine’s Day’ na huadhimishwa kila mwaka inapofi ka tarehe kama ya leo.

Hii ni siku inayoadhimishwa na watu mbalimbali na kwa mitindo tofauti huku wengine wakiipindua ‘kichwa chini miguu juu’ na kuifanya ipoteze maana kusudiwa.

Katika mazungumzo na gazeti la HabariLEO, watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, taasisi, wasomi na vijana wanaeleza namna jamii inavyoitazama na hata wengine kuiadhimisha kwa mtindo wa kutii amri ya kijeshi ya ‘nyumaaa geuka!’ au mtindo wa kichwa chini, miguu juu.

Asili ya Siku ya Wapendanao
Vyanzo mbalimbali vinasema historia ya Siku ya Wapendanao (Valentine’s Day) inaanzia Karne ya 3 katika Dola ya Warumi kumkumbuka, Padri Valentine aliyeuawa na Utawala wa Kirumi kwa sababu ya kutetea waumini wake kufunga ndoa, badala ya kuishi kama vimada.

Valentine anaheshimiwa kama mtakatifu na kukumbukwa tarehe hiyo. Sehemu nyingi ulimwengu huisherehekea kama siku ya mapenzi kinyume cha dhamira ya Mtakatifu Valentine anayekumbukwa na kuheshimiwa kwa namna ya kipekee kama Mtakatifu kila Februari 14.

Mmoja ananukuu mtandao wa www.history.com ukisema Kiongozi (Kaisari) wa kipindi hicho alikuwa Claudius II. Aliweka sheria kwa askari wote kutooa wala kufunga ndoa kwani aliamini askari mkakamavu ni yule asiyeoa wala kuwa na familia.

Aidha, Warumi waliamini vijana hao wangeoa, wasingekuwa na uhuru kwenda vitani, bali kuwa na famiia zao ndio maana vijana wengi walikuwa na mtindo wa kuwa na vimada tu kitu ambacho kanisa lilikukwa linapinga.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Padri Valentine alipinga sheria hiyo na kuendelea kufungisha ndoa kwa siri akihimiza vijana kufunga ndoa, badala ya kufanya ngono bila ndoa kwani ni dhambi.

Alikuwa anafungisha ndoa kwa siri kwenye makatakombe (mahandaki chini ya kanisa ambako kuna sehemu za ibada kwa watu wachache). Alifanya hivyo kwa vile kufunga ndoa hadharani ilikuwa kukiuka amri ya wakuu wa Dola ya Kirumi.

Baadhi ya watu walifichua siri hiyo na Mfalme Claudius II alipopata habari hizi aliamuru, Valentinus akamatwe na anyongwe, hivyo aliuawa kama shahidi mfiadini kutetea waumini wake wafunge ndoa badala ya maisha ya ngono bila ndoa.

Akiwa gerezani kabla ya kunyongwa, Padri Valentine aliandika barua iliyokuwa na salamu zake za kwanza kwa binti aliyekuja kumsalimia. Mwisho wa barua aliandika: ‘Kutoka kwa Valentine wako’. Toka hapo Valentinus anakumbukwa kama mtetezi wa wapendanao na Sikukuu yake huadhimishwa karibu duniani kote Februari 14.

Makosa na mambo yapasayokufanyika
Katika maadhimisho ya Siku ya Wapendanao, mara nyingi wanaume wamekuwa wakifanya makosa kadhaa huku wao wakiyaona ni mambo ya kawaida kumbe yana athari mbaya katika uhusiano wao hasa wa kimapenzi.

Andiko moja mtandaoni linamnukuu mtaalamu wa mambo ya saikolojia ya mapenzi, Dk Terri Orbuch akisema zaidi ya asilimia 75 ya wanawake wanapenda kupewa zawadi zaidi kuliko wao wanavyopenda kutoa.

Linasema wanaume wengi wamekuwa wakishindwa kuwanunulia zawadi kutokana na fikra potofu wakidhani zawadi nzuri ni kubwa pekee na za thamani kubwa ndizo zitaweza kumpa heshima.

Wataalamu zaidi wa saikolojia ya mapenzi wanasema wanaume wanapaswa kutambua na kuzingatia kuwa, wanawake hufurahia zaidi zawadi hata kama ni za kawaida na za gharama ndogo kama chokoleti na maua pamoja na kuambiwa maneno matamu ya kimahaba.

Uchunguzi wa kisaikolojia umebaini kuwa, wanawake wengine hupenda kujibu mapigo kwa wanaowanunulia zawadi hivyo, zawadi za kawaida humsaidia mpenzi/mpendwa wako hata asiyekuwa na uwezo mkubwa, naye kukununulia
kama hiyo maana wengi wana tabia ya kurudisha zawadi inayofanana na uliyomnunulia.

Siku hii ni nafasi na wakati mpya na mzuri zaidi kila mmoja kusikiliza mwenzie kwa mipango ya familia. Inaelezwa kuwa nchini Marekani, takribani asilimia 64 za wanafamilia hutumia siku hii kupanga uzazi kwa kusikiliza mipango ya mwenza.

Chanzo kinasema, “Hutumia siku hii kuombana msamaha na kuondoa migongano iliyowahi kutokea na kwa kufanya hivyo, siku hiyo huwa ya furaha kwa wapendanao.” Kinaongeza: “Kumsikiliza mwenzio huonesha namna unavyomjali”.

Kuhusu anavyojua siku hii, Mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Mawasiliano ya Umma katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Victoria Mungure anasema kila mmoja ana namna yake ya kuiadhimisha siku hii.

Anasema, “Wengi hasa vijana wameielekeza zaidi katika upendo wa kimapenzi na hawakumbuki kabisa suala la kuwapo ndugu na wazazi. “Mtu mwingine anaona kama hana mpenzi, afadhali amtafute kwa jasho kwa ajili ya siku hiyo yaani, wanafanya kosa la kuanzisha uhusiano wa kimapenzi kwa ajili ya siku hiyo huku siku hiyo pia, ikisababisha wengine kuuvuruga au kuvunja uhusiano wao.”

Anasema kosa hili hutokana hasa na baadhi ya wanawake ambao bila kujali sababu, mtu asipoalikwa na mpenzi wake kwenda matembezi maarufu ‘mtoko’ au kama hajanunuliwa zawadi au kumposti kwenye mitandao ya kijamii, anaona kama hapendwi.

Kutokana na dhana hiyo, ananuna na hata kuamua kutafuta mwingine kama namna ya kumwadhibu mwenzake. “Hili ni kosa maana upungufu wa siku moja haupaswi kufuta mazuri yote ya nyuma,” anasema. Mungure anaongeza:
“Unajua, wanawake wengi wanaishi na ugonjwa wa kuiga na kuongozwa na maisha ya mitandaoni kwenye utandawazi bila kujua hayo si maisha yao halisi…”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) ambaye pia, ni Katibu Mkuu wa Taasisi ya Mashehe na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Shehe Hamisi Mataka anasema kosa wanalofanya wengi tangu vijana hadi watu wazima, ni kusubiri kuona au kupima upendo katika siku
hii moja.

Anasema, “Katika Uislamu upendo, huruma, ushirikiano, msaada, msamaha, amani na utulivu ni mambo ya siku zote na wakati wote… Kwetu hili jambo halipo na kila wakati ni dini inataka upendo kwa umma.”

Paroko wa Parokia ya Mwanga, Jimbo Katoliki la Singida, Padri Deogratius Makuri anasema kwa Kanisa, siku hii
inalenga kukumbushana na kuhimizana zaidi umuhimu wa Upendo wa Agape yaani, upendo wa kujitoa kwa faida ya wengine.

Anasema, “Valentine ni siku ya kukumbushana na kuhimiza upendo zaidi kwa wanandoa na wanafamilia kukaa, kula na kunywa pamoja na kupanga mipango huku wakitafakari upendo wa Mungu huku wakisisitiza na kuzingatia upendo, msamaha na uadilifu katika ndoa, familia na jamii kwa ujumla na si kutekwa na kutawaliwa na tamaa za mwili.”

Padri Makuri anasisitiza, “Kama hujaoa au kuolewa katika siku hii, endelea kuwa mwaminifiu kwa usafi wa moyo na kama umeoa au kuolewa, endelea kudumisha uaminifu na upendo wako katika ndoa yaani kuendelea kulinda Amri ya Sita ya Mungu isemayo Usizini.”

Anapoulizwa kuwa mtu mmoja anapaswa kuwa na ‘Valentine’ wangapi katika siku hiyo, Mwandishi wa Habari wa Gazeti la HabariLEO, Eva Sindika anasema kwa mshangao: “Haaa! Kwani kwenye mahusiano unakuwa na wangapi, si mmoja.”

Anaongeza: “Kwenye moyo anatakiwa awepo mtu mmoja unaempenda kimapenzi, lakini pia upendo mwingine mkubwa ni kwa ndugu, jamaa na marafiki wakiwamo wazazi…” Chanzo kimoja kinaandika mtandaoni: ‘… Siku hii imekuwa ya tofauti kimapokeo kwa wapendanao na wale ambao bado wanasaka wapenzi.’

Kinasema kwa wapenzi au wanandoa, huitumia kukumbushana upendo na kupeana zawadi na kutafakari masuala ya maisha yao.

“Hawa sina habari nao maana wao huwa ni sahihi kufanya hivyo… Nipo na wale wanaotumia mwezi huu kutapeli wanawake kimapenzi. “Wengine ni hawa ambao ni vidume wenye kiu na ngono… Kama kuna kipindi ambacho wadada ‘wanatumika’ ni hiki maana wanaume wanajua udhaifu wao ni vijizawadi na mtoko.”

Mmoja aliyekataa kutaja jina anasema, “Watu wamegeuza siku hii na kuifanya kuwa hatari na inayokinzana na juhudi za mapambano ya kutokomeza ukimwi… “Ni siku ambayo watu wanatumia vibaya pesa na kubaki wanasumbua wenzao kwa mikopo huku wakijaa malalamiko kuhusu hali ngumu… Bahati mbaya, siku hiyo baadhi ya wanawake wanajigeuza na kuwa ‘kausha damu’ kwa wanaume wenye uhusiano nao.”

Wasemavyo wengine
Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Kutetea Uhai (HLI) kwa Kanda ya Afrika kwa Nchi zinazozungumza Kiingereza, Emil Hagamu anasema siku hii pia itumike kuimarisha uhusiano usioweza kuvunjika kati ya mwanamke
na mtoto aliyemo tumboni mwake.

Anasema, “Upendo huo ukiimarishwa, hapatatokea mama kumuua mtoto wake kabla au baada ya kuzaliwa.”
Hagamu ambaye pia, ni Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (Prolife) Tanzania, alisema uhusiano mwingine
mzito ni kati ya mume na mke unaojengeka katika misingi ya kuaminiana na kusitiriana.

“Mume asiyempenda mke wake atamsema vibaya ndani na nje ya ndoa yao na mke asiyempenda mume wake,
atamsema vibaya mbele ya watu,” anasema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wanahabari Watetezi wa Uhai na Familia (JOLIFA), Frida Manga anasema, “Watu
wasitumie siku hii kuharibu utu wao kwa kujiingiza kwenye mapenzi kabla au nje ya ndoa… Siku hii itumike katika
maana ile ambayo mwasisi wake (Mtakatifu Valentine) aliifanya kuonesha upendo kwa wahitaji zaidi wakiwamo
wagonjwa, yatima na makundi mbalimbali ya watu.”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button