Mkoa wa Morogoro katika historia ya ukombozi Afrika

MOROGORO ni miongoni mwa miji michache nchini yenye umaarufu kutokana na mchango wake kwenye harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.

Miongoni mwa mambo yaliyofanywa kwenye mji huo wakati wa harakati hizo ni pamoja na jukumu la kuandaa kambi na vyuo vya wapigania uhuru wa nchi mbalimbali za Afrika.

Hatua hii ilitokana na jitihada za Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliunga mkono harakati za ukombozi wa Afrika akiwa na lengo la kuiona Afrika yenye umoja kwa imani kuwa bara hilo haliwezi kuwa na umoja kama nchi zake zote hazijawa huru.

Akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1984 hadi 1985 na Mwenyekiti wa nchi za mstari wa mbele wa ukombozi wa Afrika, Mwalimu Nyerere alielekeza baadhi ya maeneo nchini, ikiwemo Morogoro yaandaliwe kuwa vituo vya wapigania uhuru wa Afrika.

Umaarufu wa Mji wa Morogoro kwenye harakati hizo ulitokana na mwanasiasa mkongwe, Anna Abdallah ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa mkoa.

Kwenye moja ya maelezo yake alipokuwa Morogoro anaeleza alivyopokea ujumbe wa Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afika ulioongozwa na Brigedia Jenerali Hashim Mbita akiwa na ujumbe wa Chama cha African National Congress (ANC).

Anna Abdallah anasema Afrika Kusini kwa wakati huo walikuwa wakinyanyaswa kwa watoto wao kutopewa elimu, wakati mwingine elimu ya kiwango cha chini, hali iliyofanya vijana kufanya mapinduzi na kuishia kuwa wakimbizi.
Anaeleza kuwa wakati huo ANC iliamua kuwachukua vijana wao na kuwatawanya kwenye nchi mbalimbali kwa ajili ya kuwatafutia elimu katika ngazi mbalimbali kuanzia elimu ya msingi hadi ya juu.

“Walitafuta na baadaye waliangukia Tanzania na walipofika Tanzania wakati ule tulikuwa na Kamati ya Ukombozi chini ya Brigedia Jenerali Hashim Mbita,” anaeleza mama Anna Abdallah.

Anansema kati ya maeneo yaliyofikiriwa, kamati hiyo iliona Morogoro ndiyo inafaa kutokana na kuwa na mashamba mengi yaliyokuwa yametelekezwa, yakiwemo ya Dakawa yaliyokuwa yakilimwa mazao ya mahindi na Mazimbu yaliyokuwa ya Mkonge.

“Nikiwa RC (Mkuu) wa Mkoa wa Morogoro ujumbe wa Afrika Kusini na wa kamati ya ukombozi walifika kuniona na kuniomba maeneo,” anasema Anna Abdallah. “Kwanza tulifikiria kuwapekela Tarafa ya Matombo, Wilaya ya Morogoro, … tukaona ni mbali na jinsi ya kufika huko ilikuwa kazi ngumu, tukaangalia eneo la Kingolwira na hapo tulipaona pana matatizo kwa sababu ya kuwepo kwa makambi makubwa ya wapigania uhuru,” anasema.

Anaeleza baada ya kuhangaika ikaamuliwa waoneshwe Mazimbu eneo ambalo lilikuwa linamilikiwa na wananchi kwa shughuli za kilimo baada ya wamiliki wake wa awali kuyaacha. Anaeleza kuwa uamuzi wa kuanzisha Kambi ya
Dakawa ulitokana na idadi kubwa ya vijana kwenye eneo la Mazimbu hali iliyolazimu kuamuliwa kuwatengenisha
wakubwa na vijana.

Anasema eneo la Dakawa yalikuwa ni mashamba ya mahindi na baada ya kuamuriwa kujenga kambi hiyo, Chama cha ANC kilichukua jukumu la kutengeneza Barabara, kuvuta umeme, kuchimba visima, ujenzi wa majengo na kuwahamishia watu wazima kutoka kambi ya Mazimbu.

Ofisa Michezo na Utamaduni Mkoa wa Morogoro, Grace Njau anaeleza kuwa mkoa huo una vituo vinne ambavyo vilihusika na masuala ya ukombozi.

Anavitaja vituo hivyo kuwa ni ANC Dakawa kilichopo Wilaya ya Kilosa, ANC Mazimbu kilichopo Manispaa ya Morogoro na kituo cha mafunzo kwa ajili ya wauguzi ambao walitumika kuwahudumia wapigania uhuru ambapo kwa sasa maeneo hayo yanatumika kama makazi ya Askari Polisi.

Kituo kingine ni Kingolwira Mkumbo kilichopo Manispaa ya Morogoro. Mmoja wa madaktari wazalendo, Salum Mwandu ambaye alishiriki katika harakati za kuhakikisha wapigania uhuru wanapata elimu ya utabibu katika chuo
cha kitaifa cha utabibu kwa wanaharakati za ukombozi kilichokuwa mkoani humo, anaelezea namna mambo
yalivyokwenda.

Dk Mwandu anaeleza kuwa vyama vyote vya ukombozi Kusini mwa Afrika ikiwemo NPLA (Angola), SWAPO (Namibia), ANC na PAC (Afrika Kusini), ZANU PF na ZAPU (Zimbabwe) pamoja na FLELIMO cha Msumbiji, vilikuwa na Ofisi Dar es Salaam na makada wao walipata mafunzo ya ukombizi wa nchi zao nchini Tanzania.

Dk Mwandu anasema chuo hicho kilianzishwa kwa wazo la Umoja wa Mataifa chini ya utekelezaji wa Mwalimu Nyerere.

Anasema chuo hicho kiliitwa kwa jina la United Nations Health Assistance to Southern African Liberations
Movement na kilianzishwa mwaka 1976 hadi 1985 kikiwa na jukumu la kutoa kozi za uuguzi, wataalamu wa maabara, waganga wa meno, waganga wasaidizi na watumishi wa nyanja nyingine za afya mahususi kwa vyama
vya ukombozi pekee.

Dk Mwandu anasema kuwa vyama vya ukombozi vilivyoanzishwa kutoa wanafunzi ni pamoja na ANC, PAC vya Afrika Kusini, SWAPO cha Namibia na ZANU PF cha Zimbabwe.

“Nilikuwa ni mmoja wa madaktari watatu waanzilishi wa chuo hicho ambao wawili sasa ni marehemu aliyekuwa anawasilisha Umoja wa Afrika-OAU (wakati huo) na mwingine kutoka Liberation Movement akitokea Chama cha ANC,” anasema Dk Mwandu.

Dk Mwandu anasema chuo hicho kilikuwa na jukumu la kutoa wataalamu wa maabara, waganga wa meno, madaktari wasaidizi na wauguzi wa vyama vya ukombozi Barani Afrika kwa ajili ya kwenda mstari wa mbele kusaidia mapambano ya ukombozi wa nchi zao.

Naye Mkuu wa Chuo cha Ualimu Dakawa, Dorothy Mhaiki anaeleza historia eneo la Dakawa kuwa lilikabidhiwa kwa ANC mwaka 1982 baada ya lile la Mazimbu kuonekana dogo na halikidhi mahitaji ya chama hicho.

“Eneo hili lina makaburi 52 ya waliokuwa wapigania uhuru wa ANC, uwanja wa mazoezi ya kivita na mahandaki, pia viongozi wengi wa nchi hiyo walitembelea akiwemo Nelson Mandela, Oliver Tambo na wengineo,” anasema Mhaiki.

Mhaiki anasema mwaka 1992 baada ya hali ya kisiasa kuimarika nchini Afrika Kusini na wanachama wengi
kurejea kwao, makazi ya Dakawa yalikabidhiwa kwa Serikali ya Tanzania kama kumbukumbu ya mshikamano na urafiki kati ya ANC na watu wa Tanzania.

Anasema kwa sasa eneo hilo linatumika kwa matumizi ya taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kituo cha ANC,
Chuo cha Ualimu Dakawa, Veta Dakawa, Shule ya Sekondari Dakawa, Shule ya Msingi Dakawa na Zahanati.

Mhaiki anataja baadhi ya majukumu ya kituo hicho kuwa ni kuhifadhi na kutunza mazingira, kutunza na kuhifadhi kumbukumbu za kihistoria za ukombozi wa wapigania uhuru wa Chama cha ANC cha Afrika Kusini.

“Kituo cha Maendeleo Dakawa kina jukumu la kutunza hizo kumbukumbu kwa sababu ndani ya kituo kuna
kumbukumbu kadhaa za kihistoria zikiwemo nyaraka mbalimbali zilizotumiwa na wapigania uhuru hao,” anasema.
Mhaiki anaeleza kuwa ni muhimu kuimarisha na kutunza Historia ya Ukombozi kwa kukifanya kituo hicho
kuwa kivutio cha utalii wa kihistoria.

Anasema hatua hiyo ni pamoja na kujenga makumbusho na uhifadhi wa vitabu na nyaraka zilizoachwa na wapigania uhuru ili wanafunzi wapate kusoma na kuielewa historia ya ANC sambamba na kusaidia wataalamu katika kazi za utafiti wa historia ya ukombozi wa Afrika Kusini .

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi akiwa katika ziara kwenye Kituo cha Dakawa anasema Serikali kupitia wizara yake itaweka jitihada kwa baadhi maeneo yenye historia ya ukombozi na Afrika kuyapa thamani yake.

Anasema moja ya njia za kuyapa thamani ni kuyaingiza kwenye orodha ya urithi wa Dunia chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO). Profesa Kabudi anasema maeneo yapatayo 260 ya kihistoria ya ukombozi wa Afrika yameweza kubainiwa nchi nzima.

Anayataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Dakawa na Mazimbu yaliyopo mkoani Morogoro, Kongwa mkoani
Dodoma, Mgagao Mkoa wa Iringa, Nachingwea mkoani Lindi pamoja na Bagamoyo mkoani Pwani.

“Lengo letu na sisi kama Taifa maeneo haya yaingizwe katika orodha muhimu na moja ni orodha ya urithi wa
Kimafaifa,” anasema Profesa Kabudi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button