Tuwe makini, tuelewe taratibu kabla ya kukopa

WATAALAMU wa fedha wanasema kwamba mikopo ni moja ya nyenzo ya kusaidia kupiga hatua katika nyanja za kiuchumi iwe kwa taifa au mtu mmoja mmoja.

Kwamba mikopo inasaidia katika kufanikisha maendeleo ya taifa au mtu binafsi, kwa sababu inasaidia katika kuongeza uwezo wa kifedha wa mhusika na hivyo kutimiza jukumu alilokusudia kikamilifu.

Lakini licha ya ukweli huo, kwamba jambo kubwa linalosisitiza kabla ya kuchukua mkopo, ni kufahamu wajibu na haki zao muhimu wanapotaka mkopo. Na hili limekuwa tatizo katika siku za karibuni hapa nchini kwa wakopaji hasa binafsi.

Ndio maana mitaani kumeibuka majina mbalimbali ya mikopo kutokana na maumivu wanayopata wakopaji kwa kutoelewa masharti ya mikopo hiyo.

Mikopo umiza, mikopo kausha damu ni baadhi ya majina machache yaliyopewa mikopo inayotolewa na vikundi mbalimbali nchini, ambayo wakopaji wamekumbana na masharti magumu.

Wizara ya Fedha pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika siku za karibuni wamekuwa wakitoa elimu kuhusu masuala la fedha hasa eneo la mikopo kwa nia ya kuwanusuru Watanzania wengi ambao wamekabiliwa na matatizo baada ya kuchukua mikopo kwa sababu tu hawakuelewa au kusoma vizuri masharti yake.

Kwa mujibu wa BoT, watu wengi wanaendelea kuumia kwa kukosa uelewa wa wajibu na haki zao muhimu wanapotaka mkopo na kwamba licha ya kuwepo kwa kanuni bora, sheria na sera za fedha, bado watu wanaendelea kuumia.

Katika semina iliyofanyika wiki hii mkoani Dar es Salaam, BoT imesema kwamba katika utafiti walioufanya wamebaini kinachosababisha watu kuendelea kuumia ni ukosefu wa uelewa kuhusu mambo muhimu na haki zao wanapokwenda kuchukua mkopo.

Imesema hiyo imetokana na kukutana na watoa huduma wasio waaminifu.

Tunaipongeza Wizara ya Fedha na BoT kwa ujumla kwa kuona umuhimu wa kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala ya fedha hasa mikopo kwa sababu hali mitaani ni mbaya kwani mikopo hiyo imesababisha watu kunyanyasika, kudhulumiwa na hata kutweza utu wao kwa sababu ya mikopo yenye masharti yasiyoeleweka.

Sisi tunaamini kuwa kampeni hizi zitasaidia kuwaamsha wananchi ambao bado wako katika usingizi mzito linapokuja suala la mikopo, na hivyo kuwaokoa katika kuendelea kudhulumiwa na kunyanyasika kwa sababu ya uelewa mdogo wa masuala ya fedha.

Ni muhimu kwa wakopaji kuwa makini kwa kujishughulisha kufahamu taasisi hizi zinazokopesha kama zimesajiliwa kwa mujibu wa sheria za BoT ili kuwa katika nafasi nzuri ya kufidiwa fedha zao endapo itabainika taasisi hizo zimekiuka sheria.

Kama tulivyoeleza awali kukopa si dhambi, lakini muhimu ni kufahamu wapi unakopa na unakopa kwa masharti gani ili wakati wa kurejesha fedha kusiwe na sintofahamu kwa sababu tu masharti yanaonekana kuwa magumu au hayakueleweka.

Tunaziomba pia taasisi ya fedha kama BoT iendelee kutoa elimu hii ya fedha kwa wananchi ili wafahamu haki na wajibu wao katika kukopa, lakini pia ziwe kali kwa taasisi zilizopewa leseni na zile zisizo na leseni zibanwe, ili zifuate sheria badala ya kuwakandamiza wananchi kwa sababu tu hawana uelewa mkubwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button